• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kingi bila hiari kubanana na Joho ndani ya Azimio

Kingi bila hiari kubanana na Joho ndani ya Azimio

MAUREEN ONGALA NA VALENTINE OBARA

UBABE wa kisiasa kati ya Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, na mwenzake wa Mombasa, Bw Hassan Joho, unatarajiwa ndani ya Muungano wa Azimio la Umoja One-Kenya, baada ya jaribio la chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kuondoka katika muungano huo kugonga mwamba.

Imebainika kuwa, baadhi ya maamuzi yaliyofanywa na Azimio ambapo wanachama wa PAA hawakujumuishwa katika mabaraza na kamati za muungano huo ni miongoni mwa sababu zilizoudhi chama hicho cha Bw Kingi.

Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi, ambaye amepangiwa kuwania ugavana Mombasa kupitia kwa PAA, alidai kuwa chama hicho kinabaguliwa katika Azimio kwa kiwango kinachoweza kuathiri maazimio yao kwa Wapwani.

Dkt Kingi alisema mipangilio ya muungano huo ambapo chama cha PAA hakikujumuishwa, ni ishara ya ubaguzi dhidi yao.

“Kusema ukweli matakwa yetu hayajachukuliwa kwa uzito katika muungano wa Azimio la Umoja. Tulikuwa na imani na matumaini kuwa yangeshughulikiwa tukiwa hapo ndani,” akasema.

Wiki iliyopita, Gavana Kingi alithibitisha kuwa PAA ilikuwa na nia ya kuondoka katika Azimio kwa lalama kuwa muungano huo haujali matakwa ya chama hicho.

Bw Kingi na wanachama wake walionekana kutengwa katika uwakilishi wa Pwani ndani ya muungano huo unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, kwani hawakupewa nyadhifa za uongozi.

Baadhi ya wanasiasa wa Pwani waliopewa nyadhifa katika muungano huo ni Bw Joho, ambaye ni mwanachama wa baraza la Azimio, na Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko, ambaye ni naibu mweka-hazina.

Mbali na wawili hao ambao ni wanachama wa ODM, Mbunge wa Taveta, Dkt Naomi Shaban (wa chama cha Jubilee) pia ni mwanachama wa baraza la Azimio.

Kwa upande mwingine, Katibu wa Baraza la Maimamu na Wahubiri, Sheikh Mohamed Khalifa, alichaguliwa miongoni mwa wanachama saba wa jopo la kumtafutia Bw Odinga mgombea-mwenza.

Mmoja wa wale waliotajwa kuzingatiwa kwa nafasi ya mgombea mwenza ni Bw Joho. Magavana Joho na Kingi wanatumikia kipindi cha mwisho cha ugavana katika kaunti zao.

Msajili wa vyama vya kisiasa, Bi Ann Nderitu, alitupa nje ombi la PAA kujiondoa katika Azimio, pamoja na lingine sawa na hilo lililokuwa limewasilishwa na chama cha Maendeleo Chap Chap kinachoongozwa na Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua.

Aliarifu maafisa wa vyama hivyo kuwa ni lazima watimize matakwa ya makubaliano ya Azimio.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vyama tanzu vimezuiwa kuondoka miezi sita kabla Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, na chama chochote kinachotaka kuondoka kitafanya hivyo tu angalau miezi mitatu baada ya uchaguzi.

Chama kinachotaka kuondoka lazima kiwasilishe notisi ya siku tisini kwa baraza la Azimio.

Mgombeaji ugavana Kilifi kwa tikiti ya PAA, Bw George Kithi, alilalamika kuwa, tangu wajiunge na muungano huo, hawajaridhishwa na jinsi wanavyotazamwa kama chama kidogo.

“PAA haikujiunga na muungano huo kama chama kidogo bali kwa msingi sawa na vyama vingine tanzu. Ni lazima Azimio la Umoja ituchukulie kama chama chochote kile katika muungano huo la sivyo hatuna biashara yoyote ya kufanya na watu ambao wanatuchukulia kama chama kidogo,” akasema Bw Kithi.

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Shule za upili ambazo si maarufu zadhihirisha...

Biashara zanoga Waislamu wakisherehekea Idd-Ul-Fitr

T L