• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
KINYUA BIN KINGORI: Vyama vya kisiasa vinavyoendesha ukabila visisajiliwe

KINYUA BIN KINGORI: Vyama vya kisiasa vinavyoendesha ukabila visisajiliwe

Na KINYUA BIN KINGORI

KULINGANA na Katiba, Kifungu 91 (2) (a) kinasema kuwa chama cha kisiasa hakitabuniwa kwa misingi ya dini, lugha, mbari, kabila, jinsia au eneo.

Katiba pia inaeleza chama hakipaswi kujihusisha katika kampeni za kusambaza chuki za kikabila au kisiasa. Kila wakati uchaguzi mkuu unapokaribia, viongozi wa kisiasa nchini hujitokeza kupigia debe kubuniwa kwa vyama vya kisiasa, wakisingizia kuvitumia kama chambo cha kutetea maslahi ya jamii au kabila lao kisiasa.

Inatamausha kuona vigogo wa kisiasa ambao wameishi kupinga Wakenya kujiunga na vyama vya kikabila, ndio wanaongoza juhudi za kubuniwa kwa vyama sampuli hiyo.

Viongozi hao sasa wamekuwa wafadhili wa kusaidia maeneo fulani kuanzisha vyama vyao – yote ikiwa ni kwa manufaa yao kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao.

Vitendo hivyo vinafaa kututia hofu na wasiwasi tunapoelekea debeni 2022, ikizingatiwa kuwa nchi hii imewahi kukumbukwa na ghasia za kikabila kutokana na tabia ya wanasiasa kuchochea watu kwa misingi ya kabila lao.

Je, ikiwa wanasiasa ndio huchochea ghasia za kikabila, hali itakuwaje kukiwa na vyama vya kikabila na kimaeneo nchini?

Ingawa si kosa kwa kiongozi yeyote yule kubuni chama cha kisiasa, wanasiasa wanafaa kuweka kipaumbele juhudi zao katika kuchangia amani, umoja na kudumisha utaifa, kwa kubuni vyama ambavyo ujumbe na kaulimbiu yao zinaashiria utaifa.

Kubuni chama kwa lengo la kuwakilisha jamii ya Mlima Kenya, Nyanza, Pwani, Ukambani, Magharibi, Kaskazini Mashariki au Bonde la Ufa ni sawa na kubuni vyama vya kimaeneo ila kwa njia za kiujanja.

Je, mbona wanasiasa wanakiuka mwongozo unaofaa kuzingatiwa kuanzisha vyama vya kisiasa?Je, mamlaka husika za serikali zinajua kubuniwa kwa vyama hivyo ni sawa na kuwatia hofu wananchi wa makabila mengine wanaoishi maeneo husika?

Kifungu hicho cha Katiba katika Ibara ya (2b) kinaeleza wazi kuwa, chama cha kisiasa hakitajihusisha na uchochezi wa ghasia au vitisho kwa wanachama wake, wafuasi, wapinzani au mtu mwingine yeyote.

Tumesikia baadhi ya wanasiasa wakisisitiza kuwa mwaniaji anayetaka kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao katika eneo fulani, lazima ajiunge na chama cha kisiasa kinachohusishwa na eneo hilo au jamii fulani ya hapo.

Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa iwe macho kabisa kipindi hiki ili kuvikataa vyama vinavyobuniwa kutekeleza maslahi ya kibaguzi ya jamii fulani wala havina sifa za kitaifa.

You can share this post!

Korti yaamuru raia wa Tanzania anayeishi uingereza akamatwe...

Serikali inavyokiuka Katiba kuacha raia wafe njaa