• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Kivumbi chanukia Jubilee ikijipanga

Kivumbi chanukia Jubilee ikijipanga

Na FRANCIS MUREITHI

KINYANG’ANYIRO cha ugavana wa Kaunti ya Nakuru kimechukua mwelekeo mpya, kufuatia tangazo la Rais Uhuru Kenyatta juzi kwamba chama cha Jubilee kitafufuliwa na kupewa sura mpya.

Kaunti hiyo bado inasawiriwa kuwa ngome ya Jubilee licha ya kwamba viongozi wengi wamejiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Awali, kinyang’anyiro cha ugavana kilionekana kama mbio za farasi wawili kati ya gavana wa sasa Lee Kinyanjui na Seneta Susan Kihika.

Lakini kuzinduliwa kwa mpango wa kufufuliwa kwa Jubilee, sasa kunamaanisha kwamba chama hicho kitadhamini mgombeaji ugavana kupambana na wawili hao.

Ingawa inakisiwa kuwa Bi Kihika atapewa tiketi ya moja kwa moja katika UDA, Bw Kanyanjui ambaye ni kiongozi wa chama cha Ubuntu Peoples Forum, ambacho kiko ndani ya Azimio la Umoja, atalazimika kung’ang’ania tiketi ya kuwania ugavana chini ya muungano huo, na mwaniaji kutoka Jubilee.

Bw Kinyanjui anapania kuwa gavana wa kwanza katika kaunti hiyo, yenye makabila mengi, kuhifadhi kiti chake licha ya upinzani mkali kutoka kwa Seneta Kihika.

Wadadisi wa kisiasa katika kaunti ya Nakuru wanasema Gavana Kinyanjui, ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta, ndiye ana nafasi kubwa ya kupata tiketi ya Azimio la Umoja kutetea kiti chake.

Hata hivyo, haitakuwa kazi rahisi kwake ikizingatiwa kuwa wafuasi wa Jubilee katika kaunti ya Nakuru wamegawanyika.

Mwanasiasa mkongwe Koigi Wamwere ambaye ametangaza kuwa atawania useneta wa Nakuru kwa tiketi ya Azimio la Umoja, anasema kufufuliwa kwa Jubilee sasa kumebadili mkondo wa siasa katika kinyang’anyiro cha ugavana.

“Atakayepata tiketi ya kuwania ugavana wa chini ya Azimio atateuliwa kwa kuzingatia rekodi ya maendeleo na weledi wa mwanasiasa katika kuvutia wapiga kura. Gavana Kinyanjui anaonekana kuwa na sifa hizo, hali inayoongeza uwezekano wake kupata tiketi hiyo,” akasema Bw Wamwere ambaye ni mbunge wa zamani wa Subukia.

Tayari msomi, Dkt Stanley Karanja ametangaza kuwa atawania ugavana wa Nakuru kwa tiketi ya Jubilee.

Ameahidi kupambana vikali na wawaniaji wowote ambao watajitokeza kusaka tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja kuwania ugavana wa Nakuru.

“Nataka kuwa mpeperusha bendera ya muungano wa Azimio. Nina matumaini kwamba nitashinda katika kura ya mchujo,” akasema Dkt Karanja ambaye aliwania kiti cha ubunge cha Nakuru Mjini Mashariki katika uchaguzi mkuu wa 2013.

Katika uchaguzi mkuu wa 2017, Dkt Karanja alikuwa mgombeaji mwenza wa Seneta James Mungai katika kinyang’anyiro cha ugavana kama wagombeaji wa kujitegemea.

Kwa upande wake, Gavana Kinyanjui ameonyesha matumaini kwamba atapata tiketi ya Azimio la Umoja kutetea kiti chake.

“Nitatetea kiti changu kama gavana wa Nakuru kwa tiketi ya chama cha Ubuntu Peoples Forum (UPFP),” akasema.

You can share this post!

Kalonzo amkalia ngumu Raila

Mlipuaji aua watu 13 katika hoteli Somalia

T L