• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kalonzo amkalia ngumu Raila

Kalonzo amkalia ngumu Raila

VALENTINE OBARA NA BRIAN OCHARO

JUHUDI za kuunda muungano kati ya Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na mwenzake wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, zimeendelea kupata vikwazo hata baada ya wawili hao kukutana Mombasa, Jumapili.

Viongozi mbalimbali wamekuwa wakijaribu kuwashawishi waelekee kwa uchaguzi ujao wakiwa pamoja, bila kufua dafu.

Bw Odinga, ambaye ndiye kinara wa Muungano wa Azimio La Umoja, na Bw Musyoka aliye mmoja wa vinara wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA), walikutana Jumapili asubuhi katika hoteli moja jijini Mombasa.

Ingawa Bw Musyoka alisema mkutano wao haukuwa wa mashauriano rasmi, tukio hilo lilijiri wakati ambapo duru zimesema mikakati imezidishwa ili aungane na Bw Odinga kabla uchaguzi wa Agosti.

“Ikiwa mazungumzo yatafanywa, yatakuwa ya wazi wala si mambo ya kichinichini kwa sababu tuna taifa la kujali,” akasema, katika mkutano wa hadhara Kisauni.

Alishikilia msimamo wake kwamba OKA haitamezwa na muungano mwingine huku akitaka viongozi wengine ndio wajiunge na OKA.

“Sisi hatuna shida, lakini itabidi wao wenyewe Azimio waje wajiunge nasi. Sio eti Kalonzo kila wakati ndiye ajiunge nao,” akasema.

Alikuwa ameandamana na vinara wenza wa OKA akiwemo Kiongozi wa KANU aliye pia Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi, na mwenzake wa Narc Kenya, Bi Martha Karua.

Kufikia sasa, OKA haijatangaza atakayepeperusha bendera ya muungano huo kwa urais. Bw Musyoka anataka hakikisho kwamba hawatalazimishwa kumuunga mkono Bw Odinga.

Akizungumza Jumapili, Bw Odinga alisema mikataba itakayofanywa na vyama ambavyo vitajiunga na Azimio La Umoja ndiyo itatumiwa kuamua jinsi kura za mchujo zitakavyofanywa kuamua wagombeaji uchaguzini.

“Mkataba wa Azimio utafafanua jinsi vyama vitashiriki katika mchujo. Hatutaki vyama vishindane, vigawanye kura kisha tupoteze viti. Tunataka kuona tukinyakua viti vingi zaidi katika mabunge ya kaunti na ya kitaifa,” akasema Bw Odinga, huku akiomba Wakenya wawe na subira kuhusu suala la watakaowania urais.

Miungano hiyo miwili inatarajiwa kuendeleza kampeni zao katika kaunti nyingine za Pwani ikiwemo Kwale na Taita Taveta leo Jumatatu.

Katika mahojiano ya awali, Bw Musyoka alikuwa ameapa hawezi tena kushirikiana na Bw Odinga uchaguzini akidai kuwa, waziri huyo mkuu wa zamani amemsaliti mara nyingi walipoungana katika chaguzi zilizopita.

Alipohutubu katika mkutano wa hadhara Kaunti ya Nyamira wiki iliyopita, Bw Musyoka alidokeza angependa kuwe na muungano mkubwa utakaowawezesha kushinda uchaguzi wa urais katika raundi ya kwanza.

Bw Odinga jana Jumapili aliongoza kikosi chake hadi uwanja mkubwa wa Tononoka kwa mkutano wa hadhara, huku Bw Musyoka akielekea Kisauni.

OKA ilikuwa imetaka kutumia uwanja wa Tononoka lakini ikabainika dakika za mwisho kwamba Azimio La Umoja, ilikuwa tayari imepewa leseni ya kuandaa mkutano katika uwanja huo.

  • Tags

You can share this post!

Kingi amezewa ODM ikimkwaza

Kivumbi chanukia Jubilee ikijipanga

T L