• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Mlipuaji aua watu 13 katika hoteli Somalia

Mlipuaji aua watu 13 katika hoteli Somalia

Na MASHIRIKA

BELEDWENYE, Somalia

WATU 13 waliuawa Jumamosi nchini Somalia, baada ya mlipuaji wa kujitoa mhanga kujilipua kwenye mkahawa uliojaa wanasiasa na maafisa wa ngazi za juu serikalini.

Kulingana na msemaji wa polisi Dini Roble Ahmed, wengi kati ya wale waliofariki ni raia.

Mlipuko huo ulifanyika katika mji wa Beledwenye, eneo la Kati.

Polisi walisema jumla ya watu 20 walijeruhiwa kwenye mlipuko huo.“Kando na maafa, mlipuko ulisababisha uharibifu mkubwa,” akasema Roble.

Wale walioshuhudia walisema mlipuko ulitokea katika eneo la wazi kwenye mkahawa wa Hassan Dhiif, ambako watu wengi walikuwa wamekusanyika kula chakula cha mchana.

“Niliona miili ya watu kadhaa. Singeweza kuhesabu idadi ya majeruhi waliokimbizwa hospitalini,” akasema Mahad Osman, ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika eneo la mkasa.

Polisi na maafisa wa serikali walithibitisha kuwa shambulio hilo lilitekelezwa na mlipuaji wa kujitoa mhanga, japo hawakutoa idadi kamili ya watu waliofariki.

Shambulio hilo lilifanyika licha ya hali ya usalama mkali kudumishwa katika mji huo kutokana na uchaguzi wa bunge unaoendelea.Ripoti zilieleza kuwa miongoni mwa watu waliofariki ni manaibu wawili wa wakuu wa wilaya.

Kulingana na ripoti za kijasusi za mtandao wa SITE, kundi la wapiganaji wa al-Shabaab ndilo lililodai kuhusika.

Tovuti hiyo huwa inadhibiti taarifa za mtandaoni zinazotolewa na kundi hilo.

Kwa muda wa wiki mbili zilizopita, kundi hilo limetekeleza mashambulio mawili hatari.

Kundi hilo, ambalo huwa na uhusiano na kundi la al-Qaeda, linalenga kuipundua serikali kuu ya Somalia, inayoongozwa na Rais Mohamed Farmajo.

Chaguzi za bunge zilianza Novemba 1, 2021 ambapo zilitarajiwa kumalizika Desemba 24. Hata hivyo, sasa zimepangiwa kumalizika Februari 25.

Kulingana na taratibu za uchaguzi nchini humo, wajumbe, ambao huwajumuisha wazee wa koo huwa wanawachagua wawakilishi wa bunge la chini, ambapo baadaye watamchagua rais mpya, ijapokuwa tarehe haijatangazwa bado.

Wadadisi wanasema kuna uwezekano mashambulizi yanayotekelezwa na kundi la al-Shabaab kusababisha matatizo mengi kuhusu uchaguzi huo, ambao umecheleweshwa kwa karibu mwaka mmoja.

Hali hiyo pia inatajwa kuzitia wasiwasi nchi zinalolifadhili taifa hilo, ambapo zinahofia ucheleweshaji wa uchaguzi umekuwa ukipunguza juhudi ambazo zimekuwa zikiendeshwa kukabiliana na wanamgambo wa kundi hilo.

Mnamo Januari, msemaji wa serikali ya taifa hilo alijeruhiwa kwenye mlipuko wa bomu jijini Mogadishu.Msemaji huyo, Mohamed Ibrahim Moalimuu, alikimbizwa hospitalini mara tu baada ya shambulio hilo.

Kituo cha habari cha Serikali—Somalia Nationa News Agency (SNNA)—kilisema shambulio hilo lilitekelezwa na mshambuliaji wa kutijoa mhanga.

Ripoti zilieleza hiyo si mara ya kwanza kwa msemaji huyo kulengwa na magaidi.

Moalimuu alihudumu kama mwanahabari kabla ya uteuzi wake.

Licha ya uwepo wa majeshi ya mataifa kadhaa nchini humo kuisaidia serikali kukabiliana na wanamgambo wa al-Shabaab, wataalamu wa masuala ya usalama wanasema mzozo kati ya Rais Farmajo na Waziri Mkuu Mohamed Roble umechangia sana kudorora kwa usalama.

You can share this post!

Kivumbi chanukia Jubilee ikijipanga

Mcheza kamari wa Vietnam ashtakiwa kwa ulaghai wa Sh6.5M

T L