• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Kosgey ahimizwa awanie kiti cha useneta Nandi

Kosgey ahimizwa awanie kiti cha useneta Nandi

Na TOM MATOKE

MBUNGE wa Emgwen, Alexander Kosgey, mwana wa aliyekuwa Waziri Henry Kosgey, sasa atagombea kiti cha useneta Kaunti ya Nandi mwaka 2022.

Aidha, kakake Allan anamezea kiti cha ugavana wa kaunti hiyo.

Mbunge huyo anayehudumu kipindi cha pili, amekuwa akishinikizwa na wapigakura kugombea useneta.

Kwa wakati mmoja Gavana Stephen Sang alimuidhinisha kuwania kiti hicho kinachoshikiliwa na Seneta Samson Cherargei.

Katika mkutano ulioleta pamoja wajumbe kutoka wadi nne za eneobunge la Emgwen, walimuidhinisha rasmi Bw Kosgey kugombea useneta.

Wajumbe hao kutoka wadi za Kilibowon, Kapakangan, Chepkumia na Kapsabet walisema mbunge huyo amedhihirisha kwamba anaweza kazi ya useneta.

Wakiongozwa na Bismark Sang, Simon Yego, Japheth Kiptoo na Kennedy Kirui, walimtaka Bw Cherargei kugombea ugavana kwani amekuwa akikosoa vikali serikali ya Gavana Sang.

Licha ya himizo awanie useneta, Bw Kosgey ameshikilia kwamba malengo yake ni kuhudumia wakazi wa Emgwen.

“Miradi mingi ya maendeleo imekwama Kenya kwa sababu wapigakura wamechagua viongozi waliohusishwa na kashfa za ufisadi. Lakini Kosgey amedhihirisha kwamba ni mchapakazi na anafaa kugombea wadhifa mkubwa wa kaunti kwani uongozi wa sasa (Sang na Cherargei) umegawanyika,” Askofu Mstaafu wa ACK Eldoret, Thomas Kogo, alisema majuzi.

Mnamo Agosti, Gavana Sang alisema yuko tayari kuungana na Bw Kosgey kwa mchujo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais William Ruto mwaka 2022.

Gavana Sang ametofautiana na Seneta Cherargei na wawili hao wamekuwa mahasimu wa kisiasa uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.

You can share this post!

TSC yachunguza mwalimu kwa dai la uporaji wa pesa

Kiraitu, Munya wafufua uhasama kuelekea 2022