• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kiraitu, Munya wafufua uhasama kuelekea 2022

Kiraitu, Munya wafufua uhasama kuelekea 2022

GITONGA MARETE na DAVID MUCHUI

MAHASIMU wa muda mrefu Gavana Kiraitu Murungi na Waziri wa Kilimo Peter Munya wameanzisha upya vita vyao vya kisiasa kabla ya uchaguzi wa kuwania kiti cha ugavana Meru mwaka 2022.

Waziri Munya amejitokeza waziwazi kuashiria nia yake ya kuwania kiti cha ugavana Meru, huku akihudhuria mikutano zaidi mjini humo na kutoa taswira ya kiongozi wa kitaifa.

Kwa Gavana Murungi kinyang’anyiro hicho kitakuwa mizani kali itakayoamua iwapo angali na ushawishi wa kisiasa eneo hilo.

Wawili hao walikabiliana kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa 2017 katika kinyang’anyiro ambacho Bw Murungi alimpiku mpinzani wake huyo mkuu na kunyakua ugavana wa Meru.

Kibarua cha kupata kura za wakazi wa Meru kinafanywa kuwa kigumu kutokana na tofauti ya mitazamo na makabila ya jamii ya Wameru.

Sawa na wawaniaji wengine wanaomezea mate ugavana katika eneo la Mlima, Bw Munya – ambaye ndiye alikuwa gavana wa kwanza wa Meru – anatumai kutumia “udhaifu” wa Gavana Murungi kumbwaga kiongozi huyo wa sasa wa kaunti.

Wawili hao wameanzisha upya uhasama kati yao huku Waziri Munya akipuuzilia mbali hatua ya gavana kuunda chama cha kimaeneo, na kusema ameshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Bw Munya anaongoza kampeni za kumpigia debe mgombea wa Jubilee, Bw Samson Kinyua, katika uchaguzi mdogo wa Wadi ya Kiagu utakaofanyika Oktoba 14.

Amepuuzilia mbali kauli ya Bw Murungi kwamba chama cha Jubilee kimesambaratika kabisa.

Alimtaka gavana kusahau kiti cha ugavana 2022 na “kurejea Seneti” akisubiri kustaafu siasa.

Lakini Bw Murungi alijibu vikali akisema rekodi ya utendakazi wake iko wazi “kwa kila mwenye macho kujionea” na kuongeza kuwa miaka mitano ya Bw Munya alipohudumu kama gavana “haikuzaa chochote” ikilinganishwa na miaka yake minne hadi sasa.

“Baadhi ya mambo yaliyofanikishwa na serikali yangu ni kama vile uchimbaji wa visima 195 katika muda huo, kilinganishwa na visima 17 vya Munya katika miaka mitano. Tumejenga madarasa 273 ya ECDE ikilinganishwa na Munya aliyejenga 100, kando na kumalizia ujenzi wa madarasa 105 ya ECDE aliyoachia njiani,” Gavana Murungi alisema Jumanne katika makao makuu ya kaunti hiyo.

Uhasama huo mpya unaashiria mapambano makali debeni mwaka ujao huku Gavana akisema yuko tayari kumkabili Waziri.

“Acha Munya aje, simwogopi. Ikiwa kuna mtu tuna uhakika wa kumbwaga 2022 ni Munya,” alitisha kiongozi huyo wa kaunti.

Mwakilishi Mwanamke Kawira Mwangaza vilevile ametangaza nia ya kugombea kiti hicho.

Kuhusu kubuniwa kwa chama ambacho Bw Munya alisema “hakiongezi thamani kwa mwananchi” na kuwa ni kama “nyoka anayejitoa ngozi na kuwa hatari zaidi.”

Gavana alisema Bw Munya hajui lolote kuhusu siasa.

You can share this post!

Kosgey ahimizwa awanie kiti cha useneta Nandi

Mbunge atumai Gideon Moi atanyaka tiketi ya OKA