• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Kwekwe, Boga waibua joto kali ugavana Kwale

Kwekwe, Boga waibua joto kali ugavana Kwale

TANGAZO la Katibu katika wizara ya Kilimo Prof Hamadi Boga na mwenzake wa Huduma za Magereza Bi Safina Kwekwe kuwa watawania pamoja ugavana kaunti ya Kwale kwenye uchaguzi mkuu ujao limezua joto la kisiasa katika kaunti hiyo.

Gavana wa Kwale Salim Mvurya ambaye anampigia debe naibu wake Fatuma Achani anamlaumu Prof Boga na Bi Kwekwe akidai hawajaleta maendeleo licha ya kuwa serikalini.

“Wale walioteuliwa ndio hatukuwaona 2018 wakitufanyia kazi hapa Kwale. Au nyinyi mliwaona wale makatibu walioteulwia wakitufanyia kazi au kusema hapa ni Kwale zaidi?” alisema Bw Mvurya.

Wiki mbili zilizopita, Prof Boga na Bi Achani walitangaza rasmi kuwa watawania ugavana kupitia chama cha ODM. Baadhi ya wazee wa Kaya wamewatawaza Prof Boga na Bi Kwekwe wakimsihi kinara wa ODM Bw Raila Odinga kuwaunga mkono.

“Mimi na dadangu Kwekwe tuna azma ya kuwania uongozi wa Kwale 2022. Azma hii inatokana na kwamba ni nafasi ya watu wa Kwale kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi wapya sababu katiba inawaruhusu,” alisema Prof Boga.

Aliongeza kuwa ataleta maendeleo hasa katika sekta ya kilimo.“Kwale ina uwezo wa kuzalisha samaki tani laki tatu lakini bado tuko tani 1000 ambayo ni hasara na ni umasikini. Kwale ina uwezo wa kuzalisha korosho tani laki tatu hivi sasa bado tunazalisha tani 1000. Mikorosho twaiangalia miaka 10 hatukuwekeza kwenye sekta hiyo, nafasi iko ya kugeuza haya maneno,” alisema Prof Boga.

Hata hivyo katika mikutano ya siasa, Bw Mvurya amekuwa akimsuta Prof Boga kwa kushindwa kuleta mageuzi hayo kwenye wizara yake.

“Hata hii miembe na mikorosho na mambo yote ambayo alisema pale yako chini ya Wizara ya Kilimo, mbona inangoja Bw Odinga mwaka ujao isitekelezwe sasa wakati ni katibu?” aliuliza Bw Mvurya akimsuta Prof Boga.

Bi Achani aliwataka wagombea hao (Prof Boga na Bi Kwekwe) waonyeshe maendeleo yao kwa wakazi.“Siasa ni maendeleo, waje waonyeshe maendeleo yao pia. Mimi ninajua wana wasiwasi,” alisema Bi Achani.

Kufikia sasa ni wagombea watano ambao wamejitokeza wakiwemo waziri wa zamani Chirau Mwakwere (Wiper), mfanyibiashara Daniel Dena (KANU), Spika wa Bunge la Kaunti ya Kwale Sammy Ruwa (ODM) na Bw Lung’anzi Mangale.

Gavana Mvurya ambaye anahudumu muhula wake wa pili aliwaambia wakazi kumchagua Bi Achani akisema ataendeleza maendeleo ambayo serikali yao imeanzaisha.

Aliwataka wapiga kura kuchagua viongozi kulingana na maadili mema na maendeleo na kupuuzilia mbali kabila, chama na jinsia huku akiendelea kumpigia debe naibu wake.

Bi Achani ni kati ya wanawake watano wanaowania ugavana eneo la Pwani. Wengine ni pamoja na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa (Kilifi) kupitia UDA, Patience Nyange (Taita Taveta) kupitia Wiper, Umra Omar (Lamu), Ruweida Obbo (Lamu), Rachel Mwakazi (Taita Taveta).

Bi Achani ambaye aliidhinishwa na Naibu wa Rais William Ruto kugombea kiti hicho kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA) amekuwa naibu gavana tangu mwaka wa 2013.

  • Tags

You can share this post!

Wanyonge maskini wanavyopuuzwa

Viongozi wa kidini walaumu Joho kwa kuachia wafanyakazi njaa

T L