• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Viongozi wa kidini walaumu Joho kwa kuachia wafanyakazi njaa

Viongozi wa kidini walaumu Joho kwa kuachia wafanyakazi njaa

Viongozi wa Kidini na mashirika ya kijamii kaunti ya Mombasa, yamemshutumu Gavana Hassan Joho kwa kushindwa kulipa mishahara wafanyakazi wa kaunti ambao wameanza mgomo baridi.

Zaidi ya wafanyakazi 4,000 wa kaunti hawajalipwa mishahara yao tangu Novemba mwaka jana. Maafisa hao wakiwemo madaktari, walimsihi Rais Uhuru Kenyatta kuwanusuru kutokana na kile walichokitaja kuwa uongozi mbaya wa Bw Joho.

Sheikh Abu Hamza wa msikiti wa Sparki na mtetezi wa Haki za Kibinadamu Bw Julius Ogogoh, walisema hawatanyamaza wakati Gavana Joho ananyanyasa wafanyakazi. Wawili hao waliunga mkono wafanyakazi wa kaunti wapewe haki yao.

Shiekh Hamza alishutumu Gavana Joho kwa kukataa kuwalipa wafanyakazi mishahara yao ya Novemba na Disemba licha ya kutumia mamilioni ya pesa kuandaa sherehe ya kukaribisha mwaka mpya katika bustani ya Mama Ngina Water Front.

“Tunataka suluhu, lakini yasikitisha kwamba kaunti inaweza kutumia pesa nyingi kwa mambo ambayo hayana maana yoyote…kuleta waimbaji na kadhalika. Kwa nini washindwe kulipa wafanyakazi? Huduma za afya zikisitishwa matajiri watasafiri ng’ambo kwa matibabu lakini sisi wanyonge tutaumia,” alisema Sheikh Hamza.

Alisema hivi karibuni viongozi watawaomba wakazi kuwapigia kura ilhali wamenyamaza wakati wafanyakazi wanapuuzwa na serikali ya Gavana Joho. Mkutano wa kusuluhisha mzozo huo ulioongozwa na Bw Joho haukufua dafu.

“Gavana Joho alihudhuria kikao chetu cha kutafuta suluhu lakini walikataa kukubali matakwa yetu, haturudi kazini hadi pale tutakapolipwa mishahara yetu na tupewe bima ya afya,” alisema Dkt Hassan Mkuche mwenyekiti wa muungano wa madaktari (KMPDU).

  • Tags

You can share this post!

Kwekwe, Boga waibua joto kali ugavana Kwale

Wenyeji Cameroon wafungua fainali za AFCON 2021 kwa ushindi...

T L