• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 10:01 PM
Leo ni leo Mombasa na Kakamega

Leo ni leo Mombasa na Kakamega

NA WAANDISHI WETU

WAKAZI wa Kaunti za Mombasa na Kakamega, hatimaye wanatarajia kupata nafasi ya kuamua utawala mpya wa kaunti zao leo Jumatatu.

Kaunti hizo mbili zimekuwa chini ya magavana Hassan Joho na Wycliffe Oparanya mtawalia tangu serikali za ugatuzi zilipoanzishwa mwaka wa 2013.

Katika Kaunti ya Mombasa, wapigakura 641,913 waliosajiliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) watakuwa huru kujiamulia mmoja kati ya wagombeaji saba wanaoshindania urithi wa kiti cha Bw Joho.

Saba hao ni Bw Hezron Awiti wa Chama cha Vibrant Democratic Party, Bw Omar Hassan (UDA), Dkt William Kingi (PAA), Bw Daniel Kitsao (mgombeaji huru), Bw Shafii Makazi (UPIA), Bw Abdulswamad Nassir (ODM) na Bw Said Omari (Usawa Kwa Wote).

Jana Jumapili, maafisa wa IEBC walikuwa wanakamilisha mipango ya mwisho ya maandalizi ikiwemo kusafirisha vifaa vya uchaguzi hadi katika vituo ambavyo wananchi watapigia kura.

Wizara ya Elimu iliruhusu tume hiyo kutumia shule kama vituo vya kura leo Jumatatu pekee, na hivyo basi inatarajiwa shughuli zote za kupiga kura zikamilike kwa muda unaofaa ili kazi itakayobaki iwe ya kujumlisha hesabu za kura. Shule hazitatumiwa kwa shughuli hiyo.

Mkuu wa uchaguzi Mombasa, Bi Swalhah Yusuf, alisema kila wadi imepewa mtambo wa ziada wa kutambua wapigakura kielektroniki almaarufu kama KIEMS, ili kuepusha changamoto za kuchelewesha upigaji kura endapo mtambo mmoja utapata hitilafu.

“Tumethibitisha vifaa vyote viko sawa. Hapa Mombasa hakuna kituo chochote kilicho na wapigakura zaidi ya 700. Wote watatambuliwa kwa kutumia KIEMS,” akasema.

Katika Kaunti ya Kakamega iliyo na wapigakura 844,551 waliosajiliwa na IEBC, kinyang’anyiro cha kurithi kiti cha Bw Oparanya pia kimevutia wagombeaji saba.

Wao ni Bw Fernandes Barasa (ODM), Bw Shakhalaga Jirongo (UDP), Bw Suleiman Kanyanya (KANU), Bw Cleophas Malalah (ANC), Bw Samuel Omukoko (MDP), Bw Austine Opitso (mgombeaji huru), na Bw Michael Sakwa (mgombeaji huru).

Maafisa wa usalama walizidisha ushikaji doria katika kaunti hizo mbili ili kuhakikisha uchaguzi hautatatizwa kwa vyovyote vile.
Malori ya maafisa wa GSU yalionekana yakishika doria katika sehemu mbalimbali za Kakamega jana Jumapili.

Kamanda wa polisi katika kaunti hiyo, Bw Joseph Kigen, alisema walipokea ripoti kwamba baadhi ya wanasiasa walikuwa wanapanga kutatiza shughuli katika baadhi ya vituo vya uchaguzi.

Maafisa wa usalama waliweka vizuizi katika baadhi ya barabara kuu ikiwemo ile ya Kisumu-Kakamega na Kakamega-Bungoma-Busia ambapo magari yalikaguliwa kabla madereva kukubaliwa kuendelea na safari zao.

“Tunafuatilia hali kwa karibu na tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote anayepanga kutatiza uchaguzi. Hatutahurumia mtu yeyote anayejaribu kuzua fujo wakati wa uchaguzi,” akasema.

Mkuu wa uchaguzi katika Kaunti ya Kakamega, Bw Joseph Ayatah, alisema tume hiyo inashirikiana kwa karibu na idara ya usalama ili kuhakikisha uchaguzi utafanywa kwa njia huru, wazi na ya haki.

IEBC iliahirisha chaguzi hizo mara ya kwanza Agosti 9 wakati kulipokuwa na mkanganyiko wa karatasi za kura, kisha zikaahirishwa tena Agosti 23 wakati mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Wafula Chebukati, alipodai hali haikuwa salama kwa maafisa wake.

Maeneo mengine ambayo yatafanya uchaguzi leo baada ya kuahirishwa ni maeneobunge ya Rongai, Pokot Kusini, Kacheliba na Kitui Rural, na wadi za Nyaki Magharibi (Meru) na Kwa Njenga (Nairobi).

Ripoti za Valentine Obara, Winnie Atieno na Benson Amadala

  • Tags

You can share this post!

Mombasa, Kakamega debeni leo

TAHARIRI: Waajiri wasinyime wafanyakazi wao ruhusa ya...

T L