• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Maandamano: Raila akunja mkia

Maandamano: Raila akunja mkia

CHARLES WASONGA Na MARY WANGARI

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga amefutilia mbali mkutano aliopanga kuuongoza leo Jumatano katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi siku moja baada ya Rais William Ruto kuonya mrengo huo dhidi ya kuchochea fujo nchini.

Muungano huo sasa umesema mkutano huo utafanyika Desemba 7 katika uwanja huo huo wa kihistoria, baada ya mitihani ya kitaifa kukamilika.

“Tumeahirisha mikutano yetu ya mashauriano hadi Desemba 7 kutokana na mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na ile ya Gredi 6 (KPSAE) inayoendelea,” kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi aliwaambia wanahabari baada ya mkutano wa kundi la wabunge wa Azimio (PG) katika makao makuu ya Wiper, Karen, Nairobi.

Mkutano huo uliongozwa na Bw Odinga na kuhudhuriwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Mlezi wa chama cha DAP-Kenya, Eugene Wamalwa.

Mnamo Jumatatu, Rais William Ruto alimuonya Bw Odinga dhidi ya kuongoza maandamano nchini kwa kisingizio cha kupinga kutimuliwa kwa makamishna waasi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wao ni; Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, na makamishna Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi.

Walipinga matokeo ya uchaguzi wa urais uliotangazwa na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati wakidai kutohusishwa katika hatua za mwisho za ujumuishwaji kura.

Bw Odinga alitangaza, akiwa Kisumu wiki jana kwamba, mkutano wao wa kwanza aliotaja kama wa kusaka maoni kuhusu pendekezo la kufurushwa kwa Cherera na wenzake, ungefanyika Nairobi, kisha iandaliwe miji ya Mombasa, Kisumu, Nakuru na Kakamega.

Lakini Rais Ruto alionya kwamba mikutano hiyo haifai kwani inaweza kuvuruga amani nchini na kuleta migawanyiko miongoni mwa Wakenya.

“Sidhani kwamba kufanya maandamano ni sehemu ya njia za kuifanya serikali iwajibike. Nataka niwaonye ndugu zetu katika upinzani dhidi ya kuchochea ghasia nchini,” akasema alipozuru kampuni ya kutengeneza vyakula, Twiga Foods mjini Ruiru, Kiambu.

Lakini Bw Odinga alishikilia hivi: “Tutasaka mashauriano mapana na Wakenya wote. Tutawauliza ikiwa watakubali kufutwa kwa makamishna hao wanne wa IEBC. Baada ya hapo tutatoa mwelekeo.”

“Bado sijasema mengi. Nitaongea siku zijazo. Lakini hatua ya kwanza ni kuwazuia watu hawa kuwafuta kazi makamishna hao. Nitakabiliana na serikali hii bila woga,” Bw Odinga akaongeza.

Mnamo Jumatatu, kundi dogo la wanachama wa Bunge la Mwananchi lilifanya maandamano nje ya ukumbi wa County ambako Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) imekuwa ikifanya vikao vya kuchambua maombi yanayopendekeza kung’olewa kwa Bi Cherera na wenzake.

Wakiongozwa na Rais wa vuguvugu hilo, Calvin Okoth, wanaharakati hao waliishutumu serikali ya Rais Ruto kwa kuongozwa na haja ya kulipiza kisasi dhidi ya Bi Cherera na wenzake.

“Rais Ruto aachane na Cherera na wenzake ambao hawakufanya hatia yoyote kwa kusimama na ukweli wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. Ruto apunguze bei ya unga badala ya kuwaandama makamishna wasio na hatia,” akasema.

Lakini jana Jumanne, viongozi wa muungano wa Wafanyabiashara wa Nairobi (NBC) waliapa kulinda biashara zao ili zisiharibiwe katika maandamano yatakayoongozwa na vinara hao wa Azimio.

Wakiongea na wanahabari jana Jumanne, viongozi wa muungano huo wakiongozwa na mshirikishi wao Benson Mutura hata hivyo, walisema wanachama wao wako tayari kupambana vikali na waandamanaji wa Azimio.

“Tunamwomba Raila kufutulia mbali maandamano hayo kwa sababu yanaweza kuharibu biashara zetu. Hata hivyo, tungependa kuwaonya kuwa tuko tayari kupambana nao ikiwa watathubutu kusababisha machafuko na hivyo kuharibu biashara zetu,” akaeleza Bw Mutura, ambaye ni Spika wa zamani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi.

Wakati huo huo, kundi la wanasiasa kutoka Luo Nyanza jana Jumanne walipinga mpango wa Azimio kuitisha maandamano sehemu mbalimbali nchini wakisema, vijana kutoka jamii hiyo ndio wataumia.

“Ikiwa ni lazima wafanye maandamano, basi tunawatawa waweke watoto wao mstari wa mbele. Na watoto wao wasivalie vesti za kuzuia risasi au mawe,” Gavana wa zamani wa Kisumu Jack Ranguma akawaambia wanahabari katika mkahawa mmoja jijini Nairobi.

Aliandamana na Seneta wa zamani wa kaunti hiyo Fred Outa, Mbunge wa zamani wa Rangwe Martin Ogindo, miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Mafunzo ya marefarii wa Ligi ya Taifa Divisheni ya Kwanza...

Tunisia ina kibarua kulaza Ufaransa leo Jumatano

T L