• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Magavana waanza kazi kwa kishindo

Magavana waanza kazi kwa kishindo

NA WAANDISHI WETU

MAGAVANA 45 walioapishwa katika kaunti mbalimbali nchini Alhamisi iliyopita walianza kazi jana kwa kishindo huku wakazi katika kaunti husika wakiwa na matarajio makuu kuhusu usimamizi mpya.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia, Gavana George Natembeya aliwasili afisini mwake saa moja asubuhi, pengine kama ishara ya kutuma ujumbe mkali kwa wafanyakazi wa kaunti.

“Leo nilifika afisini mwangu saa moja asubuhi. Naamini na ninatumai wafanyakazi wote wa kaunti watatilia maanani hali mpya iliyoanza,” alisema Bw Natembeya katika kikao na wanahabari afisini mwake.

“Ni vyema kufahamu kuwa kazi ya kaunti si ya lazima hivyo mtu anapopewa fursa ya kutoa huduma, tunatarajia ajitolee kwa dhati.”

Gavana wa Murang’a, Irungu Kang’ata, alianza kazi kwa kupiga marufuku ununuzi wa bidhaa za matibabu kutoka kwa mashirika ya kibinafsi.

Akizungumza Jumatatu katika siku yake ya kwanza afisini, Bw Kang’ata aliagiza bidhaa hizo zinunuliwe tu kutoka kwa Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA).

“Ni ghali kwa wagonjwa kununua dawa kwenye maduka ya nje. Kaunti itanunua dawa kutoka kwa KEMSA hatua itakayoondoa mawakala na ulaji rushwa. Itapunguza vilevile kiasi cha pesa zinazotumiwa kununua dawa na kuhakikisha zinapatikana katika vituo vyote vya afya,” alisema.

Katika Kaunti ya Nyandarua gavana Kiarie Badilisha aliamuru wagonjwa wote waliozuiliwa katika Hospitali ya JM kuhusiana na bili za matibabu waachiliwe mara moja.

Alipozuru ghafla hospitali hiyo, gavana alihuzunika aliposikia jinsi wagonjwa wamezuiliwa katika kituo hicho cha afya kwa miezi zaidi ya mitatu.

“Inasikitisha na ni ukatili kumzuilia binadamu hospitalini. Haina maana kwangu kwa sababu wanachukua nafasi ya hospitali ambayo ingetumiwa na umma. Ni mateso kiakili, kiroho na kihisia kwa wagonjwa na jamaa, wanapaswa kuwa nyumbani wakifanya kazi kulisha na kuelimisha watoto wao,” alisema.

Gavana wa Kaunti ya Turkana, Jeremiah Lomorukai, mnamo Jumapili usiku alishuhudia binafsi alichotaja kama hali duni iliyokithiri katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti kufuatia kilio cha muda mrefu kutoka kwa umma kuhusu huduma duni.

Katika ziara ya ghafla iliyochukua muda wa saa tatu, Bw Lomorukai alishuhudia mazingira duni ambayo wagonjwa wamelazimika kustahimili ikiwemo ukosefu wa huduma za ambulensi za kuwasafirisha kuenda katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, Eldoret, upungufu wa wahudumu pamoja na vitanda.

“Hospitali ipo katika hali duni kwa sababu katika baadhi ya wadi wagonjwa wanalazimika kulalia vitanda visivyo na magodoro huku wengine waliolazwa katika wadi zenye misongamano wakilala sakafuni,” alisema mkuu huyo wa kaunti.

Gavana wa Kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga naye atalazimika kutumia mamilioni kununua magari mapya yatakayotumiwa na maafisa wakuu katika serikali yake kwa shughuli rasmi.

Ripoti za Waikwa Maina, Sammy Lutta, George Odiwuor Na Martin Mwaura

  • Tags

You can share this post!

Majaji 5 wa kigeni kuhudhuria kesi

Paul ‘Mamba’ Chebor ang’oa Moi katika...

T L