• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Magavana waliofaulu Agosti 9 waapishwa kuingia ofisini

Magavana waliofaulu Agosti 9 waapishwa kuingia ofisini

NA SAMMY WAWERU

MAGAVANA wateule 45 wanaapishwa leo Alhamisi ili kuchukua rasmi hatamu za uongozi wa kaunti, baada ya kuchaguliwa Agosti 9, 2022.

Tayari wananchi wamefika katika nyanja za shughuli hiyo, kushuhudia magavana na manaibu wao wakilishwa kiapo na majaji.

Serikali za kaunti zilianza utendakazi 2013, baada ya kupitishwa na kuidhinishwa kwa Katiba ya sasa 2010.

Kenya ina jumla ya kaunti 47, zinazoongozwa na magavana. Aidha, kila kaunti ina baraza lake la mawaziri, wanaoteuliwa na gavana.

Miaka 10 baada ya kuzinduliwa kwa serikali za ugatuzi, baadhi ya maeneo yameandikisha ukuaji mkubwa hasa miundomsingi kama vile barabara, sekta ya afya, kilimo, miongoni mwa nyinginezo.

“Yapo baadhi ya maeneo haswa yale kame, awali hayakuwa na barabara bora wala vituo vya afya. Kwa sasa, wanaridhia huduma hizo kupitia ugatuzi,” akasema Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa.

Bw Wamalwa hata hivyo ametaja kero ya ufisadi kuwa ni miongoni mwa changamoto kuu zinazozingira utekelezaji wa ugatuzi hivyo kuhujumu nia ya kila mwananchi kupata huduma za serikali.

“Ufisadi unatishia ugatuzi,” akaonya Waziri huyo, akizungumza mapema Alhamisi katika Kaunti ya Trans Nzoia alikofika kushuhudia kuapishwa kwa gavana mteule George Natembeya.

Ili kuafikia malengo ya serikali za kaunti, Bw Wamalwa alishauri magavana kutilia maanani maendeleo.

“Pia kaunti zianze kuzalisha mapato yake badala ya kutegemea serikali kuu,” akashauri.

Gavana wa Tharaka Nithi, Muthomi Njuki tayari ameapishwa kuhudumu muhula wa pili.

Bw Njuki alilishwa kiapo dakika kumi na tano baada ya saa nne asubuhi.

  • Tags

You can share this post!

Wajackoyah ajitolea kumsaidia kijana aliyewania ubunge

Kiapo: Johnson Arthur Sakaja aanza majukumu ya Gavana...

T L