• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Magavana wanaohepa Azimio waelezea hofu

Magavana wanaohepa Azimio waelezea hofu

BENSON MATHEKA Na SHABAN MAKOKHA

MAGAVANA wa Azimio la Umoja-One Kenya ambao wamekuwa wakikwepa mikutano ya hadhara kupinga utawala wa Rais ya serikali, sasa wanataka viongozi wa muungano huo wa upinzani wakome kuwashambulia kwa kuisusia.

Magavana wengi wa muungano huo wamejitenga na mikutano na wito wa maandamano wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wakisema wanashirikiana na serikali kwa ajili ya maendeleo.

Baadhi yao wamefika Ikulu kukutana na Rais William Ruto na wamekuwa wakihudhuria hafla zake.

Hata hivyo viongozi wa Azimio wamekuwa wakitumia mikutano hiyo kuwalaumu wakidai wamewekwa makwapani na serikali.

Magavana ambao hawajahudhuria mikutano ya ‘maasi’ ya Raila Odinga katika kaunti zao ni Dkt Wilbur Ottichilo wa Vihiga, Bw George Natembeya (Trans Nzoia), Dkt Paul Otuoma (Busia), Bw Amos Nyaribo (Nyamira) na Bi Wavinya Ndeti (Machakos).

Bw Odinga amekuwa akiongoza washirika wake kuwashambulia magavana wanaosusia mikutano ya Azimio inayoandaliwa katika kaunti zao.

Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka aliwataka wafuasi wake eneo la Ukambani wapuuze viongozi ambao wamegeuka na kuunga mkono serikali.

“Ni ukahaba wa kisiasa kwa mtu ambaye alichaguliwa kwa tikiti ya ODM, Wiper, Jubilee au chama chochote tanzu ndani ya Azimio la Umoja kujiunga na Kenya Kwanza,” akasema Bw Musyoka.

Bi Ndeti amekuwa akiambia wakazi wa kaunti yake ya Machakos kwamba, ana haki ya kushirikiana na serikali ya Rais Ruto kwa ajili ya maendeleo ya kaunti yake na kwa hivyo viongozi wa Azimio hawafai kumlaumu kwa kususia mikutano wanaoandaa.

Akihutubia wakazi wa kaunti ndogo za Kathiani na Yatta, Bi Ndeti aliwataka wakazi kumuunga mkono katika juhudi zake akisema anafaa kutumia muda kuwahudumia na sio kwenye mikutano ya hadhara kwa kuwa “uchaguzi ulimazika na ni wakati wa kufanya kazi.”

Aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, ambaye ni naibu kiongozi wa ODM, alinukuliwa akisema hatua ya magavana hao ni dharau kwa muungano huo na vyama ambavyo walichaguliwa kwa tikiti yake.

“Nilikuwa mbunge miaka 10, nikawa gavana kwa miaka mingine 10 na nilifanikiwa kufanikisha miradi kwa raia bila kuenda ikulu. Magavana wana bajeti. Kwa nini wanakimbia ikulu kwa madai ya kupata maendeleo?” akauliza.

Bw Odinga ameongoza mikutano minane tangu mwezi Januari ambapo ametangaza kuwa hatambui uhalali wa serikali ya Rais William Ruto, akidai kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka jana haukuwa na uwazi.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha katika Baraza la Magavana, alisema kuwa magavana wana mikataba ya kufanya kazi na Rais Ruto ili kuimarisha maendeleo katika maeneo yao.

Bw Barasa alimpinga Bw Oparanya akisema alifanikiwa sana wakati wa utawala wake kwa sababu wakati huo alishirikiana na utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

MDD kushika Raila mkono Pwani huku Ruto akizidi kupenya

Deni la maziwa ya Sh71m latia kaunti ya Mombasa mashakani

T L