• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
MDD kushika Raila mkono Pwani huku Ruto akizidi kupenya

MDD kushika Raila mkono Pwani huku Ruto akizidi kupenya

NA JURGEN NAMBEKA

KIKUNDI cha Movement for the Defense of Democracy (MDD), kilichozinduliwa hivi majuzi na Kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, sasa kinataka jukumu la kumwandalia mikutano yake eneo la Pwani.

Wiki iliyopita, Bw Odinga alitarajiwa kufanya mkutano wa hadhara Mombasa lakini mpango huo ukabadilika, afisi yake ilipodai kuwa hatua hiyo ya kuuahirisha ingetoa nafasi ya maandalizi kabambe zaidi.

Rais William Ruto, ndiye aliyezuru maeneo ya Pwani wikendi hiyo ikiwemo Kaunti ya Mombasa ambapo aliendelea kuwarai viongozi na wananchi wanaoegemea upande wa Upinzani kuungana na serikali yake.

Duru zilisema Bw Odinga anatarajiwa Pwani wiki hii, ingawa hajathibitisha. Wakizungumza katika kikao na wanahabari jana, wanachama wa vuguvugu la MDD tawi la Mombasa waliwakashifu baadhi ya viongozi wa Azimio eneo la Pwani kwa kutokuwa waaminifu kwa Bw Odinga.

“Kama MDD tawi la Mombasa, tunataka kumhakikishia kinara wetu Bw Odinga kuwa tuko naye. Watu wamekuwa wakipewa peremende na vitamu kutoka kwa serikali ya kitaifa ili kuyumbisha ngome hii lakini sisi hatubanduki,” akasema Bw Peter Otieno, mwenyekiti wa vuguvugu hilo eneobunge la Nyali.

Vinara wa ODM wamekuwa wakiwalaumu baadhi ya magavana kwa kutojitolea kuendeleza mbele ajenda za chama huku wakionekana kuelekeza uaminifu wao kwa serikali ya Kenya Kwanza.

Naibu Mwenyekiti wa ODM, Bw Wycliffe Oparanya, wiki iliyopita aliwakashifu magavana na wanasiasa wengine wa Upinzani wanaokwepa mikutano ya Azimio.

“Kiongozi ni lazima awe na msimamo. Baadhi ya viongozi walichaguliwa kupitia Azimio lakini wanaendelea kuenda Ikulu wakijifanya wanatafuta maendeleo. Wewe ukiwa gavana, ni maendeleo gani unayoenda kutafuta katika Ikulu ilhali una bajeti yako?” akauliza.

Bw Oparanya, aliye gavana mstaafu wa Kakamega, aliwataka wafuasi wa Azimio kuwazia upya viongozi aina hiyo akidai wana ubinafsi.

Jana Alhamisi, wanachama wa MDD walisema hawawezi kulegeza msimamo wa kuunga mkono nia ya Bw Odinga kupigania haki na maisha bora kwa wananchi.

Bi Judith Odira, mmoja wa wanachama wa vuguvugu hilo, alieleza kuwa kupanda kwa gharama ya maisha kumewaacha wananchi wakihangaika.

Wanachama hao walipuuzilia mbali madai ya Kenya Kwanza kuwa Bw Odinga anapoteza umaarufu wake eneo la Pwani kwa chama cha UDA kinachoongozwa na Rais Ruto.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa ODM tawi la Nyali, Bw Fadhili Mzee, chama hicho kitawapa matumaini wafuasi kuwa kingali imara iwapo kitaandaa mikutano yake Pwani.

Alisema watahakikisha Bw Odinga amefika katika maeneo ya vitongoji duni kama vile Dunga Unuse na Kaa Chonjo ili kusemezana na wananchi waliompigia kura moja kwa moja.

Walikuwa wameandamana na aliyekuwa diwani wa wadi ya Tudor, Bw Samba Tobias, aliyetarajiwa kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi baada ya mahakama kubatilisha ushindi wa Bw Samir Baloo.

Bw Odinga amenuia kufanya mikutano ya hadhara katika miji yote mikuu nchini kabla ya kupanga maandamano ya kushinikiza serikali ya Rais Ruto, kutekeleza matakwa mbalimbali.

Miongoni mwa matakwa ya Azimio ni kuwa serikali ipunguze gharama za bidhaa muhimu, na kubadili mtindo wa kuajiri makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

  • Tags

You can share this post!

NCPB yakumbwa na upungufu wa mahindi licha ya kupandisha...

Magavana wanaohepa Azimio waelezea hofu

T L