• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Magavana wapya wanarithi madeni na mzigo mkubwa wa mishahara

Magavana wapya wanarithi madeni na mzigo mkubwa wa mishahara

NA CHARLES WASONGA

MADENI, bajeti kubwa ya mishahara, miradi iliyokwama na migomo ya wafanyakazi ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili magavana 37 wapya wanaoingia afisini leo Alhamisi, Agosti 25, 2022.

Hawa ni miongoni mwa magavana 45 ambao wanaapishwa  kufuatia ushindi wao katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Miongoni mwa magavana  hao ni; Susan Kihika (Nakuru), Johnson Sakaja (Nairobi), James Orengo (Siaya), Jonathan Bii (Uasin Gishu), Jeremiah Lomurkai (Turkana), Kiarie Badilisha (Nyandarua), Jonathan Leleliit (Samburu) na Irungu Kang’ata (Murang’a).

Wengine ni; Fatuma Achani (Kwale ), Simon Kachapin (West Pokot), Ochilo Ayacko (Migori), Wisley Rotich (Elgeyo Marakwet), Kimani Wamatangi (Kiambu), Simba Arati (Kisii), Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na Andrew Mwadime (Taita Taveta).

Magavana hawa wanaoanza kuhudumu muhula wa kwanza wanakabiliwa na madeni ya kima cha Sh130 bilioni ziliachwa na watangulizi wao.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya uongozi mizigo ya madeni ambayo magavana hao wapya wamerithi itaathiri uwezo wao wa kutekeleza miradi ya maendeleo waliyoodhesha katika manifesto zao.

“Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Sheria za Usimamizi wa Fedha za Umma, 2012, itawalazimu kulipa madeni hayo, japo uhalali wa madeni mengine ni wa kutiliwa shaka,” anasema Bw Barasa Nyukuri.

Kaunti ya Nairobi ni miongoni mwa zile ambazo zinazongwa na mzigo mkubwa wa madeni.

Kulingana na ripoti kuhusu Utekelezaji wa Bajeti katika Serikali za Kaunti (CGBR) kaunti ilikuwa na madeni ya kima cha Sh84.94 bilioni kufikia Juni 30, 2022.

Kaunti zingine zenye madeni makubwa ni kama vile, Kiambu (Sh5.21 bilioni), Mombasa (Sh4.82 bilioni), Wajir (Sh3.82 bilioni), Machakos (Sh2.80 bilioni) na Tana River (Sh2.41 bilioni).

Magavana wapya pia watakumbana na bajeti kubwa ya mishahara ya wafanyakazi hali ambayo itaathiri uwezo wao wa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kwa mfano, katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022 kaunti nyingi zilielekeza fedha nyinyi katika matumizi yasiyofungamana na maendeleo kama vile ulipaji mishahara ya wafanyakazi.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Msimamizi wa Bajeti Dkt Margaret Nyakang’o Juni 2022, kaunti zilizotumia pesa nyingi kwa matumizi yasifungamana na miradi ni; Nakuru, Samburu, Baringo, Narok, Kericho, Trans Nzoia, Uasin Gishu, West Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet na Laikipia.

  • Tags

You can share this post!

Kiapo: Johnson Arthur Sakaja aanza majukumu ya Gavana...

Mwanamume seli kujaribu kujiua sababu ya deni

T L