• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Vitendo vya Uhuru vilivyomjenga Ruto

Vitendo vya Uhuru vilivyomjenga Ruto

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta alifanya msururu wa makosa yaliyompa nguvu na kumjenga kisiasa naibu wake, William Ruto, akidhani alikuwa akimkata kucha kupunguza umaarufu wake.

Wawili hao walitofautiana katika kipindi cha pili cha utawala wa serikali ya Jubilee na Dkt Ruto na washirika wake wakatengwa serikalini na chamani.

Hii ilimfanya Dkt Ruto kuunda chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho ni moja ya vyama vikubwa vya kisiasa vinavyomezewa mate kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Wadadisi wa siasa wanasema makosa ambayo Rais Kenyatta alifanya ni kukumbatia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ambaye alikuwa mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, na kuvunja ahadi yake kumuunga Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wakati wa handisheki Machi 9, 2018. PICHA | MAKTABA

“Hatua ya Rais Kenyatta ya kumkumbatia Bw Odinga kupitia handisheki yao na kuvunja ahadi yake wakati wa uchaguzi kwamba angemuunga naibu wake kuwa mrithi wake 2022 ilifanya umaarufu wa Dkt Ruto kuongezeka kote nchini,” asema mdadisi wa siasa Peterson Kariuki.

Anasema hatua hii ilifanya umaarufu wa Dkt Ruto kuongezeka eneo la Mlima Kenya ambalo kwa miaka mingi limekuwa likimchukulia Bw Odinga kama hasimu wa kisiasa.

“Wapigakura wa Mlima Kenya walimchukulia Rais Kenyatta kama msaliti kwa kuvunja ahadi yake ya kuhudumu kwa miaka kumi na kisha amuunge Dkt Ruto atawale kwa miaka kumi. Imekuwa ni mlima kwa Rais Kenyatta kushawishi wakazi wa eneo hilo kuwa handisheki haikuwa ya kumhujumu naibu wake,” asema mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

Utafiti wa hivi punde wa kampuni ya Infotrak unaonyesha kuwa, Dkt Ruto ndiye mgombea urais maarufu eneo la Mlima Kenya kwa asilimia 46.

Kulingana na Kariuki, makosa mengine ambayo Rais Kenyatta alifanya yakamjenga zaidi Dkt Ruto ni kumtenga katika serikali yake na katika chama tawala cha Jubilee. Mwaka mmoja baada ya kuanzisha Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao Dkt Ruto alipinga, Rais Kenyatta aliwaondoa washirika wa Dkt Ruto katika nyadhifa za uongozi bungeni na katika chama tawala na kujaza nafasi hizo na washirika wa Bw Odinga na chama cha Kanu kinachomuunga mkono.

Miongoni mwa waliotemwa ni Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen ambaye pia alikuwa kiongozi wa wengi katika seneti, Susan Kihika (kiranja( seneti), Kithure Kindiki (naibu spika, seneti), Aden Duale (kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa) na Benjamin Washiali (kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa).

Washirika wa Dkt Ruto ambao wameungana naye katika UDA, pia walivuliwa nyadhifa na uanachama katika kamati za bunge na seneti.

Wadadisi wanasema Dkt Ruto na washirika wake walitumia hatua hiyo kuzidisha kampeni yao ya kujipigia debe kote nchini, wakikosoa serikali na kujenga chama chao cha UDA.

“Ruto alifukuzwa Jubilee na mtu akifukuzwa nyumba aliyojenga hana budi kujenga nyingine, alipata makao katika UDA na sasa ndicho chama kikubwa nchini. UDA inashindana na ODM ambacho kimekuwepo kwa miaka 16 iliyopita,” alisema mbunge mmoja wa Jubilee ambaye aliomba tusitaje jina akikiri kwamba kumtenga Dkt Ruto serikalini kulimjenga zaidi.

Anasema Jubilee kingekuwa chama imara kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 kama Rais Kenyatta hangetofautiana na Dkt Ruto ambaye alinuia kukitumia kugombea urais.

Dkt Ruto na washirika wake wamekuwa wakimlaumu Rais Kenyatta kwa kudanganywa na Bw Odinga kusambaratisha chama cha Jubilee.

  • Tags

You can share this post!

Hofu wazee wakipoteza pesa katika kamari

Raila aonya maafisa wa Uganda kuhusu wavuvi

T L