• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:59 PM
Masuala nyeti ya Wakenya katika uchaguzi

Masuala nyeti ya Wakenya katika uchaguzi

MWANIAJI wa urais ambaye manifesto yake itaelezea jinsi ya kuimarisha usalama nchini na kupunguza gharama ya bidhaa nchini atachukua idadi kubwa ya wapigakura milioni 3 ambao hawajaamua.

Utafiti wa kura ya maoni uliofadhiliwa na kampuni ya Nation Media Group unaonyesha kuwa masuala muhimu ambayo idadi kubwa ya Wakenya inataka yashughulikiwe ni usalama (asilimia 86), uchaguzi wa amani (asilimia 85) na kupunguzwa kwa gharama ya bidhaa (asilimia 82).

Masuala mengine ambayo Wakenya wanahitaji ni kubuniwa kwa nafasi za ajira (asilimia 82), kuangamiza ukabila (asilimia 81), kuboresha huduma za afya (asilimia 81), kuimarisha huduma za umma (asilimia 81), kupambana na ufisadi (asilimia 81), kuongoza kwa kuzingatia sheria na Katiba (81) na kupunguza deni la kitaifa (79).

Naibu Rais William Ruto anayewania urais kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA) amekuwa akisema kuwa atasaidia Wakenya wa tabaka la chini kuboresha maisha yao kupitia mfumo wake wa ‘bottom up’ kwa kuwapa mikopo nafuu.

Kwa upande wake mwaniaji wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga amekuwa akiahidi kuinua uchumi lakini hajatoa ufafanuzi wa kutosha kuhusu mbinu atakayotumia.

Bw Odinga amesema kuwa atazindua manifesto yake wiki hii. Manifesto hiyo ndiyo itatumiwa na wawaniaji wote wa muungano wa Azimio katika kampeni zao, kwa mujibu wa Bw Odinga.

Kuhusu suala la usalama, Dkt Ruto amesema kuwa atahakikisha kuwa kandarasi za kununua silaha zinazotumiwa na maafisa wa usalama, wakiwemo wanajeshi, zitawekwa wazi kama njia mojawapo ya kuzima ufisadi.

Lakini wakosoaji wake wanasema kuwa hatua hiyo huenda ikaweka nchi hatarini.

Katika mkataba wa Kenya Kwanza, Dkt Ruto ameahidi kubuni wadhifa wa waziri mkuu kupitia amri ya rais kwa ajili ya kiongozi wa Amani National Congress Musalia Mudavadi.

Kubuniwa kwa wadhifa huo kutakiuka muundo wa sasa wa serikali uliomo katika Katiba.

Bw Odinga alipokutana na jamii ya Wasomali Jumatano, aliahidi kufungua mpaka baina ya Somalia na Kenya. Lakini wakosoaji wake wanasema kuwa hatua hiyo huenda ikatoa mwanya kwa magaidi wa Al-Shabaab kushambulia nchi mara kwa mara.

Kulingana na utafiti huo uliofanywa na kampuni ya Infotrak, masuala mengine ambayo Wakenya wanataka kiongozi atakayerithi Rais Uhuru Kenyatta kuyashughulikia ni kudumisha usawa miongoni mwa jamii zote nchini (asilimia 79), kukabili makali ya mabadiliko ya tabianchi (asilimia 79) na kudumisha uhusiano mwema baina ya Kenya na mataifa ya kigeni (asilimia 78).

Aidha, utafiti huo wa Infotrak unaonyesha kuwa kwa sasa Bw Odinga na Dkt Ruto watapata asilimia 42 za kura kila mmoja iwapo uchaguzi utaandaliwa leo.

Utafiti pia unaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya wana imani kuwa Idara ya Mahakama itashughulikia mizozo ya uchaguzi kwa haki.Asilimia 72 ya Wakenya wana imani na Idara ya Mahakama, vyombo vya habari (asilimia 71), Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (asilimia 64) na Idara ya Polisi (asilimia 54).Idadi kubwa ya wakazi wa Bonde la Ufa ambayo ni ngome ya Dkt Ruto ndio wanaongoza kwa kuwa na imani kubwa na IEBC (asilimia 74) na Idara ya Mahakama (asilimia 80).

  • Tags

You can share this post!

Uchunguzi duni huvuruga kesi zinazohusu polisi – Haji

Ruto acheza karata ya mwaniaji mwenza

T L