• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Mawaziri wanaootea siasa wana kibarua!

Mawaziri wanaootea siasa wana kibarua!

NA BENSON MATHEKA

Huku Rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kubadilisha Baraza la Mawaziri wakati wowote wale wanaomezea mate viti vya kisiasa wakijiuzulu kufikia Februari 9, wa – dadisi wanasema huenda ikawa mlima kwa wakuu hao wa wizara wanaopanga kugombea viti kuvishinda.

Baadhi yao wamekuwa wakishiriki siasa licha ya kuwa katiba inawazuia mawaziri kufanya hivyo katika hatua za kujiandaa kumenyana na wapinzani wao kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Miongoni mwa wanaotarajiwa kujivua uwaziri ni Charles Keter (Ugatuzi), John Munyes (Madini na Petroli), Simon Chelugui (Leba), Peter Munya (Kilimo), Eugene Wamalwa ( Ulinzi), Ukur Yatani ( Fedha) na Sicily Kariuki (Maji). Bw Keter ametangaza kuwa atagombea kiti cha Ugavana kaunti ya Kericho kumrithi Paul Chepkwony anayehudumu muhula wa mwisho.

Wadadisi wanasemaa japo ana ukuruba wa karibu na Naibu Rais William Ruto ambaye chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) ni maarufu eneo hilo, huenda Keter akatolewa jasho na wagombeaji wa vyama vingine.

“ Si hakika kwamba atapata ushindi wa moja kwa moja kwa kuwa kuna wagombeaji wengine waliojijenga mashinani japo ni mwanasiasa mwenye uzoefu wa miaka mingi,” asema mdadisi wa siasa Kiprono Arap

Kipchirchir.

Bw Chelugui ambaye anamezea mate kiti cha ugavana kaunti ya Baringo atalazimika kufanya kazi ya ziada kuweza kumbandua Gavana Stanley Kiptis huku Bw Munya anayenuia kugombea kiti cha ugavana kaunti ya Meru akitarajiwa kutoana jasho na Gavana Kiraitu Murungi.

Bw Munyes atakuwa na kibarua katika azma yake ya kumrithi Gavana wa Turkana Josphat Nanok ambaye anakamilisha muhula wa pili huku Ukur Yatani akilenga kumbandua Gavana Ali Mohamud Mohamed.

Bw Munya na Bw Yatani ambao walikuwa magavana wa kwanza wa Meru na Marsabit mtawalia wametambua vyama vya kisiasa wanavyothibiti katika kile ambacho wadadisi wanasema kuepuka ushindani katika mchujo wa vyama vikubwa vya kisiasa.

Bi Kariuki ambaye amedokeza kuwa atawania kiti cha ugavana kaunti ya Nyandarua atazimika kutumia mikikakati ya hali ya juu kumshinda Gavana Francis Kimemia ambaye atakuwa akitetea kiti chake.

Ingawa Bw Wamalwa amekuwa akishiriki siasa haijabainika atagombea kiti kipi kaunti ya Trans Nzoia baada ya chama anachohusisha nacho cha Democratic Action Party Kenya (DAP-K) kuashiria kuwa kitamkabidhi aliyekuwa kamishna mshirikishi wa eneo la Rift Valley George Natembeya tiketi ya kugombea ugavana katika kaunti hiyo.

Waziri wa Uchukuzi James Macharia pia ameashiria kuwa atagombea kiti cha kisiasa kinachochukuliwa kuwa ugavana kaunti ya Murang’a ambapo atakuwa na kibarua kuwashawishi wapiga kura kuwakataa wagombeaji wengine akiwemo Seneta Irungu Kang’ata ambaye amekuwa akijipigia debe kwa miaka kadhaa iliyopita.

Kulingana na mdadisi wa siasa Benard Wambulwa, itategemea mrengo wa siasa ambao mawaziri hao watajiunga nao na kwa kiwango fulani rekodi yao ya maendeleo.

“Wale ambao wanamezea mate ugavana kaunti ambazo magavana wanahudumu muhula wa pili wana afueni kidogo lakini wale wanalenga kaunti ambazo magavana wanatatea viti vyao watatolewa jasho hata kama watashinda,” asema.

 

  • Tags

You can share this post!

Wazo la Raila laweza kuzima mzozo ndani ya Azimio

Upweke wajaa Ford Kenya Olago naye aking’oka

T L