• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wazo la Raila laweza kuzima mzozo ndani ya Azimio

Wazo la Raila laweza kuzima mzozo ndani ya Azimio

NA CHARLES WASONGA

HUENDA mvutano ukatokea ndani ya vuguvugu la Azimio la Umoja kufuatia tangazo la kiongozi wa ODM Raila Odinga kwamba vyama shirika vitafanya mchujo wa pamoja.

Kulingana na Bw Odinga mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa Azimio la Umoja linapata idadi kubwa ya wawakilishi katika nyadhifa za ugavana, useneta, ubunge na udiwani.

“Wale ambao watashindwa katika mchujo wasihame na kujiunga na maadui wetu. Tutawateua katika nyadhifa zingine tutakapounga serikali baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9,” Bw Odinga akasema katika makao makuu ya ODM, Nairobi baada ya kukutana na wanasiasa kutoka Kilifi.

Lakini baadhi ya vyama vinavyounga mkono ndoto ya Bw Odinga ya kuingia Ikulu kusisitiza kuwa vitadhamini wagombeaji wa nyadhifa zingine kivyao katika ngome zao.

Vyama kama vile, Pan African Alliance (PAA) chake Gavana wa Kilifi Amason Kingi, Ubuntu Peoples’ Fo – rum (UPF), kinachoongozwa Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui na Democratic

Action Party of Kenya (DAP-K), miongoni mwa mingine, vinamuunga mkono Bw Odinga.

“Baada ya kuzinduliwa kwa chama chetu cha Ubuntu Peoples’ Forum, tutaweka mikakati ya kudhamini wagombeaji katika nyadhifa zote, lakini chini ya mwongozo wa Azimio la Umoja,” Gavana Kinyanjui anasema.

Gavana huyo ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Jubilee anasema atatetea kiti chake kwa tiketi ya chama cha UPF.

Lakini makabiliano yanatarajiwa kutokea kati ya vyama vya ODM na PAA katika kaunti ya Kilifi.

Hii ni baada ya aliyekuwa mbunge wa Malindi Willy Mtengo, ambaye ni mkeretekwa wa PAA, kupendekeza ODM isidhamini wagombeaji kuanzia

wadhifa wa ugavana hadi udiwani.

“Ikiwa watafeli kutupisha na waamue kudhamini wagombeaji hapa Malindi na maeneo yote ya kaunti ya Kilifi, tutawaonyesha kivumbi,” Bw Mten – go akanukuliwa akisema.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amepuuzilia mbali pendekezo hilo la chama hicho alisema chama hicho hakitakubali pendekezo hilo.

“Bw Mtengo na chama chake cha PAA waelewe kuwa Kilifi ni ngome ya ODM na tutadhamini wagombeaji katika nyadhifa zote kuanzia ugavana hadi udiwani.

Ama kwa hakika viongozi wa PAA wanafaa kuelewa kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2017 ni katika kaunti ya Kilifi pekee ambapo ODM ilishinda viti vyote kuanzia ugavana hadi udiwani,” akasema.

Bw Sifuna anasema kufikia sasa ODM haitasaini mkataba wa maelewano na chama cha PAA “licha ya kwamba Gavana Kingi ametangaza kuwa anaunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing, ambaye anaegemea chama kipya cha Kenya United Party (KUP) naye anasema chama hicho kitadhamini wagombeaji katika nyadhifa zote kuanzia ugavana hadi udiwani.

“Kura zetu za urais zitamwendea kinara wa ODM Raila Amolo Odinga, lakini chama chetu cha KUP kitadhamini wagombeaji katika nyadhifa zingine tano; kuanzia ugavana hadi udiwani,”alisema.

 

  • Tags

You can share this post!

Sababu za Ahmed Khalif kuwa waziri kwa siku 20 pekee

Mawaziri wanaootea siasa wana kibarua!

T L