• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Mbogo adai Sonko ni ‘mpita njia’ tu

Mbogo adai Sonko ni ‘mpita njia’ tu

NA WINNIE ATIENO

UTATA wa tikiti ya mwanasiasa atakayepeperusha bendera ya Wiper katika kura ya ugavana wa Mombasa unaendelea kutokota baada ya mbunge wa Kisauni, Ali Mbogo kusisitiza kuwa kinara wa chama hicho Bw Kalonzo Musyoka alimkabidhi yeye wala sio aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko.

Bw Sonko alijitokeza kuwania ugavana wa Mombasa kupitia chama cha Wiper.

Hata hivyo Bw Mbogo alipinga akisema ni uvumi tu. Alimtaka Bw Sonko kuwaonyesha wakenya tikiti aliyokabidhiwa na chama cha Wiper kugombea nayo ugavana wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Nilipewa cheti cha muda kama mgombea wa Wiper bila kupingwa kuwania kiti cha ugavana Mombasa na kiongozi wa chama chetu Bw Musyoka kwenye ukumbi wa Bomas iliyotiwa saini na mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi Bi Agatha Solitei. Tunachosikia kuhusu Sonko ni uvumi tu. Sina mpinzani katika chama cha Wiper na hakutakuwa na uteuzi Mombasa,” akasema Bw Mbogo.

Bw Mbogo alisema mbunge wa Mvita Bw Abdulswamad Nassir ndiye mpinzani wake kwenye kinyang’anyiro hicho.

“Kama ulipewa tikiti tuonyeshe ndipo tujue kama chama cha Wiper kilitoa vyeti viwili Mombasa. Lakini ninachokijua ni kuwa Bw Mbogo ndiye atakayepeperusha bendera ya chama hapa Mombasa,” aliongeza.

Bw Mbogo, ambaye alichaguliwa mbunge wa Kisauni kwenye uchaguzi wa 2017 kupitia chama alipinga madai kwamba alijiunga na chama cha Pamoja African Alliance kinachohusishwa na gavana wa Kilifi Amason Kingi.

Wafuasi wake walimshtumu Bw Sonko kwa kuingilia siasa za Mombasa wakimtaka akagombee kiti cha siasa kaunti nyingine.

“Bw Sonko ataruhusiwa Mombasa kama atakubali kuwa mgombea mwenza wa Bw Mbogo la sivyo tutachukua hatua nyinginezo. Tunamuunga mkono Bw Mbogo,” alisema Bw Mohammed Mwajambia akiitaka chama cha Bw Musyoka kiwe na demokrasia.

Bw Mohammed Ndanda alimshtumu Bw Sonko akisema anataka kuharibu siasa za Mombasa.

“Wewe ni mkazi wa Nairobi umekuwa mbunge, seneta na gavana jiji hilo huku Mombasa hujawahi kuwa hata mzee wa mtaa,” alisema Bw Ndanda.

Wengine ambao kwenye kinyang’anyiro cha kutaka kumrithi Bw Joho ni Bw Nassir, Dkt William Kingi, PAA, na Hassan Omar UDA.

Bw Sonko alikuza siasa zake Nairobi ambako alikuwa mbunge wa Makadara kwa muhula mmoja, 2013 akawa seneta kabla ya kujitosa kwenye ugavana 2017 na kung’atuliwa na wawakilishi wa wodi ya jiji 2020 kabla hata ya kumaliza hatamu ya kwanza uongozini.

Hata hivyo, kuingia kwake katika kinyang’anyiro cha ugavana Mombasa kumetikisa siasa za eneo hilo huku wawaniaji wengine wakitazama hatua zake kwani Bw Sonko ni tishio kwa uchaguzi wao kwa sababu ya wasifu wake hasa wa kusaidia wasiojiweza.

Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi wa chama hicho Bi Solitei alithibitisha kuwa Bw Sonko ameruhusiwa kugombea ugavana baada ya kujiunga na chama hicho mwezi uliopita.

Wiper iliwasilisha jina lake kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ikisema imempitisha kuwania kiti hicho.

Uteuzi wa ugavana wa chama hicho ulikatizwa dakika za mwisho ili kuruhusu maafikiano kati ya Bw Sonko na Bw Mbogo, mgombeaji kiti cha ugavana, ambaye wiki jana alikuwa amepewa cheti cha muda cha Wiper.

Lakini Bw Mbogo alipinga akisema hawajaafikia wala kukutana na Bw Sonko kujadili swala hilo.

Bi Solitei alisema wiki iliyopita, chama hicho kilikuwa na mwaniaji mmoja wa Ugavana ambaye angelipewa tikiti moja kwa moja lakini kuingia kwa Bw Sonko ni sharti kuwe na mchujo kuchagua atakayepeperusha bendera ya Wiper Mombasa.

“Hatujapeana vyeti vya uteuzi kwa wanaowania kiti cha ugavana Mombasa kwa sababu tuna zaidi ya mgombea mmoja na hiyo ina maana kwamba itatubidi tufanya uteuzi ili kubaini mshindi,” alisema.

Makamu mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho, Bw Mutula Kilonzo Junior pia alisema orodha iliyowasilishwa kwa IEBC na chama hicho, ambayo ilijumuisha jina la Bw Sonko, ni halali.

You can share this post!

Vipusa wa Chelsea kuvaana na Man-City kwenye fainali ya...

Mbunge ataka viongozi Pwani waunge PAA

T L