• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Vipusa wa Chelsea kuvaana na Man-City kwenye fainali ya Kombe la FA msimu huu

Vipusa wa Chelsea kuvaana na Man-City kwenye fainali ya Kombe la FA msimu huu

Na MASHIRIKA

WAREMBO wa Chelsea watakutana na Manchester City kwenye fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley mnamo Mei 15, 2022 baada ya kuwapepeta Arsenal 2-0 katika mechi ya nusu-fainali mnamo Jumapili ugani Meadow Park.

Guro Reiten aliwafungulia Chelsea ukurasa wa mabao katika dakika ya 50 kabla ya Ji So-yun kucheka na nyavu za Arsenal dakika 11 baadaye.

Ingawa Arsenal walianza mechi kwa matao ya juu, walipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Vivianne Miedema na Beth Mead. Chelsea ambao ni mabingwa watetezi walishambulia Arsenal zaidi katika kipindi cha pili huku Sophie Ingle na Reiten wakimshughulisha vilivyo kipa Manuela Zinsberger.

Mechi hiyo ilikutanisha vikosi viwili vinavyoselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Uingereza (WSL).

Aidha, ilikuwa mara ya nne kwa vikosi hivyo kukutana msimu huu huku ushindi wa pekee uliosajiliwa na Arsenal ukiwa katika mchuano wa kufungua rasmi kampeni za WSL msimu huu uwanjani Emirates. Chelsea walikung’uta Arsenal kwenye fainali iliyochelewesha ya Kombe la FA msimu jana mnamo Disemba 2021 ugani Wembley.

Man-City walitinga fainali ya Kombe la FA baada ya kudengua West Ham United na watapania kuendeleza makali yao dhidi ya Chelsea baada ya kutandika kikosi hicho kwenye fainali ya League Cup mnamo Machi 2022.

Arsenal ambao ni mabingwa mara 14 wa Kombe la FA hawajashinda taji hilo tangu 2016 huku Chelsea wakilenga sasa kulitia kapuni kwa mara ya tatu chini ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kufikia sasa, ni pengo la alama moja pekee linalotenganisha viongozi Chelsea na Arsenal kileleni mwa jedwali la WSL. Walipokutana mara ya mwisho ligini, wawili hao waliambulia sare tasa uwanjani Kingsmeadow mnamo Februari 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Tulifanya kila liwezekanalo kumshawishi kocha Erik ten Hag...

Mbogo adai Sonko ni ‘mpita njia’ tu

T L