• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Mbunge wa zamani Ramadhan Kajembe afariki

Mbunge wa zamani Ramadhan Kajembe afariki

CHARLES WASONGA, FAUSTINE NGILA na WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA mbunge wa Changamwe Ramadhan Seif Kajembe amefariki Ijumaa, chama cha ODM kimethibitisha.

Mbunge wa Jomvi Badi Twalib ambaye ni mkwewe pia alithibitisha kuwa Kajembe alifariki Agosti 7, katika Hospitali ya Pandya ambako alikuwa amelazwa kwa majuma mawili akitibiwa.

Kifo cha mbunge huyo wa zamani kinajiri majuma mawili baada ya mke wake wa kwanza Mama Aziza Kajembe kufariki. Mkewe wa pili Zaharia Kajembe alifariki mnamo Machi mwaka huu.

Kulingana na taratibu za dini ya Kiislamu na kwa kuzingatia kanuni za ugonjwa wa Covid-19, mazishi ya mwendazake yatafanyika saa moja usiku katika makaburi ya familia ya Kajembe, eneo la Changamwe.

Kwenye rambirambi zake, kiongozi wa ODM Raila Odinga alisema, “Lala salama Mzee wetu mmoja wa waasisi wa chama chetu Mhe Ramadhan Seif Kajembe. Leo hii umetutangulia mbele za haki.”

“Kwa Wapwani, nasema poleni mwa msiba,” akaongeza.

Mwendazake alihudumu kama Mbunge wa Changamwe kuanzia mwaka wa 1997 hadi 2013. Kando na kuwa mbunge, alihudumu kama Naibu Waziri wa Mazingira kati ya 2008 na 2013.

Marehemu alikuwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa walioheshimiwa sana katika Kaunti ya Mombasa, ambapo aliombwa ushauri kuhusu masuala mbalimbali muhimu yanayoihusu jamii.

Vile vile alihudumu kama mwenyekiti wa Halmashauri ya Feri Kenya (KFS) kati ya 2016 na 2019.

 

Viongozi wengi walimuomboleza Kajembe huku wakisema kwamba alikuwa kiongozi wa kuigwa.

Kupitia mtandao wa Twitter Rais Uhuru Kenyatta alimwomboleza waziri huyo msaidizi wa zamani kama kiongozi mwerevu aliyetumikia nchi katika mambo tofauti .

Naibu Rais alisema kwamba, “Tumepoteza kiongozi mwenye bidii, mwenye maendeleo na aliwahudumia wananchi wake kwa ujasiri. Ramadhan alikuwa mtu mwenye malengo na mfanyakazi aliyejitolea atakayekumbukwa kwa uongozi wake mwema.”

 

You can share this post!

Wawili waliomuua mteja wa M-Pesa watafutwa

Visa vya corona sasa ni zaidi ya 25,000

adminleo