• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Mchezo wa paka na panya

Mchezo wa paka na panya

DERICK LUVEGA Na WANDERI KAMAU

MIRENGO ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja inaonekana kuchezeana mchezo wa paka na panya kuhusu mazungumzo ya maridhiano yanayotarajiwa kusuluhisha masuala tata nchini.

Hilo ni licha ya Wakenya kuelekeza macho yao yote kwa vinara wa mirengo hiyo miwili—Rais William Ruto na Raila Odinga mtawalia—kuhusu juhudi zao kutatua mzozo huo.

Hapo jana Jumatatu, wanachama watatu wa Kamati ya Malalamishi ya Bunge – wanaoegemea Kenya Kwanza – walipinga uamuzi wa kuteuliwa kwa rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obanjo, kuwa mpatanishi mkuu baina ya mirengo hiyo miwili.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Nimrod Mbai (Kitui Mashariki) na wanachama wawili; Clement Sloya (Sabatia) na Earnest Ogesi (Vihiga), walisema kuwa mzozo uliopo baina ya mirengo hiyo miwili unaweza kusuluhishwa kupitia Bunge la Kitaifa, bila kuhitaji usaidizi kutoka nchi za nje.

NIGERIA INA MATATIZO MENGI

Watatu hao walisema kuwa Nigeria, aliyoongoza Bw Obasanjo, ina matatizo mengi kuliko Kenya.

Walisema kuwa Bw Obasanjo anafaa kushughulikia matatizo hayo badala ya “masuala madogo” yanayoikumba Kenya.

Wakiongoza juhudi za kumkataa rais huyo wa zamani, Bw Mbai alimrai Obasanjo kujiondoa katika masuala yote yanayoikumba Kenya, licha ya wabunge wengi, hasa kutoka mrengo wa Kenya Kwanza, kusisitiza haja ya uwepo wa maridhiano ya kisiasa yasiyojikita kwenye ugavi wa mamlaka.

“Bw Obasanjo anafaa kuijali nchi yake ambako watu wanapigana kwa kutumia bunduki. Anafaa kushughulikia hayo badala ya kuangazia yanayoendelea Kenya, ambako watu wanaandamana kwa kutumia mawe,” akasema Bw Mbai.

Kauli za wabunge hao watatu zinajiri huku Azimio ikitangaza jana Jumatatu kundi la watu watano watakaokuwa wawakilishi katika duru ya pili ya mazungumzo ya maridhiano.

Kwenye taarifa, Azimio iliwateua Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, Seneta Okong’o Omogeni (Nyamira) na mbunge Amina Mnyazi (Malindi) kuwa wawakilishi wake. Kundi hilo litaongozwa na Bw Musyoka.

Azimio ilisisitiza kuwa msimamo wake haujabadilika kuhusu masuala itakayowasilisha.

“Msimamo wetu unabaki kuwa hakuna mrengo unaofaa kutoa masharti kwa mwingine kuhusu masuala utakaowasilisha au kutowasilisha. Azimio itaheshimu haki ya Kenya Kwanza kuwasilisha masuala yote inayotaka bila masharti yoyote. Vivyo hivyo, tunatarajia Kenya Kwanza kuheshimu yale tutakayowasilisha,” ikasema Azimio.

Mrengo huo ulisisitiza kuwa masuala utakaowasilisha ni: Kushughulikiwa kwa gharama ya juu ya maisha, usawa kwenye uteuzi wa nyadhifa kuu serikalini na serikali kuheshimu uhuru wa vyama vya kisiasa kulingana na Katiba.

Kwa mujibu wa Kenya Kwanza, masuala yanayopaswa kuwekwa kwenye mizani ni kubuniwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), utekelezaji wa sheria ya thuluthi mbili kuhusu jinsia, kuimarishwa kwa Hazina ya Maeneobunge (NG-CDF), kubuniwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani na kuingizwa kwenye Katiba kwa Afisi ya Kiongozi wa Mawaziri.

Huku Ke nya Kwa n z a ikionekana kutokuwa na haraka ya mazungumzo hayo, Azimio ilisema inatarajia kuwa mazungumzo hayo yataanza kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo Jumanne.

Mwelekeo huo mpya unajiri huku Kenya Kwanza ikiendelea kubaki kimya kuhusu watu itakaowateua kuiwakilisha katika mazungumzo hayo.

Kufikia sasa, mrengo huo umebaki kimya kuhusu ikiwa utawakilishwa na viongozi walioiwakilisha kwenye duru ya kwanza ya mazungumzo hayo au itawateua wawakilishi wapya.

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita, Bw Obasanjo aliwaleta pamoja Rais Ruto na Bw Odinga kwenye mkutano ulioripotiwa kufanyika jijini Mombasa, hali iliyotajwa kama hatua ya mwanzo ya mazungumzo hayo.

Hapo awali, Bw Odinga alikuwa amesisitiza kuwa angefanya mashauriano tu na Dkt Ruto chini ya uwepo wa mpatanishi kutoka nje.

Azimio ilidai kuwa upande wa Kenya Kwanza haujakuwa ukionyesha nia njema kwenye mazungumzo hayo.

“Kenya Kwanza haijakuwa ikionyesha nia safi katika mazungumzo hayo, na ndipo tunaweka wazi masharti na msimamo wetu. Wao ndio wamekuwa kikwazo kikuu cha mazungumzo kufanyika,” alisema aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya, kwenye kikao na wanahabari Jumapili.

Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi wanasema kuwa lazima mirengo hiyo miwili ishushe misimamo yao mikali ikiwa imejitolea kwa dhati kuhakikisha juhudi za kutafuta maridhiano zinafanikiwa.

  • Tags

You can share this post!

Dogo Valarie Nekesa ndiye mfungaji bora Divisheni 1

CHARLES WASONGA: Mpishi wa Shule ya Mukumu hakustahili...

T L