• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
CHARLES WASONGA: Mpishi wa Shule ya Mukumu hakustahili kupigwa kalamu

CHARLES WASONGA: Mpishi wa Shule ya Mukumu hakustahili kupigwa kalamu

NA CHARLES WASONGA

NAPONGEZA tume ya kupokea malalamishi kutoka kwa umma, almaarufu, Ombudsman, kwa kumtetea mpishi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Mukumu aliyefutwa kazi kwa kuwafichulia wanahabari kuhusu jinsi chakula kilichohifadhiwa visivyo kiliwasababishia wanafunzi ugonjwa na maafa.

Tume hiyo ilifanya hivyo baada habari kuhusu kufutwa kazi kwa Douglas Muchela Isutsa kuchapishwa katika vyombo vya habari wiki jana.

Kamishna wa Ombudsman, Lucy Ndung’u, alimwandikia barua Mwalimu Mkuu wa shule hiyo iliyoko Kaunti ya Kakamega, Bi Jane Mmbone, akimtaka atoe maelezo, ndani ya siku saba, kuhusu ni kwa nini Bw Isutsa alifutwa kazi.

Nakubaliana na hatua ya kamishna huyo kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Upatikanaji Habari ya 2015, mtu hafai kuadhibiwa kwa kufichua habari yenye manufaa kwa umma.

Kwa hivyo, Bw Isutsa hakufanya kosa lolote kwa kuwaelezea wanahabari jinsi nafaka na vyakula vinginevyo shuleni humo vilihifadhiwa katika mazingira machafu na ndipo vikapata sumu iliyowasababishia wanafunzi ugonjwa hatari.

Wanafunzi watatu na mwalimu mmoja waliaga dunia na wengine wengi wakalazwa hospitalini wakiendesha kutokana na athari za chakula hicho.

Kwa mtazamo wangu, Bw Isutsa ambaye alikuwa mpishi shuleni Mukumu Girls, alifichua habari hizo kwa wanahabari ili wasimamizi wachukue hatua zitakazozuia kutokea kwa mkasa sawa na huo siku nyingine.

Binafsi nimesoma maelezo ambayo mfanyakazi huyo aliyotoa kwa mwandishi wa gazeti la Taifa Leo na Daily Nation, Hellen Shikanda, baada ya mkasa wa Aprili 2023 na kung’amua kuwa hayakuwa na kasoro yoyote.

Kwa mfano, Bw Isutsa alielezea kwamba kwa mara si moja aliwahi kuwajulisha wakuu wa shule kuhusu hali mbaya ya stoo ambako chakula kilihifadhiwa lakini hawakuchukua hatua zozote.

Aliweka wazi kuwa kuta za stoo zilichibuka vibaya hali ambayo ilifanya nafaka kuingiwa na unyevunyevu ila usimamizi wa shule haukuona haja ya kukarabati kuta hizo.

Hii ina maana kuwa kulikuwa na utepetevu mkubwa kwa upande wa wasimamizi wa shule hiyo wakiongozwa na Mwalimu Mkuu aliyehamishwa, Bi Frida Ndolo.

Kwa hivyo, inasikitisha kuwa badala ya mwalimu mkuu mpya Sista Mmbone kumpongeza Bw Isutsa, yeye na bodi ya usimamizi wa shule hiyo waliamua kumpiga kalamu. Ambacho mwalimu mkuu huyo angefanya ni kuketi chini na mpishi huyo pamoja na mtangulizi wake ili wajadiliane kuhusu namna ya kurekebisha makosa yaliyotokea wakati wa uongozi wa Bi Ndolo.

Usalama wa wanafunzi ni wajibu mkuu wa wasimamizi wa shule, hasa zile za mabweni.

Kwa hivyo, ni kinyume cha utu kumfuta kazi mfanyakazi kama Bw Isutsa ambaye amesalia na miaka miwili kabla ya kustaafu.

  • Tags

You can share this post!

Mchezo wa paka na panya

Diwani ajeruhiwa kwenye shambulio la Al-Shabaab Lamu

T L