• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 10:55 AM
Mgawanyiko Azimio ikikaribia kuvunjika

Mgawanyiko Azimio ikikaribia kuvunjika

NA BENSON MATHEKA

HUKU kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga akisisitiza kwamba,upinzani hautalegeza kamba katika kukosoa serikali, dalili zinaonyesha kuwa chama cha Jubilee kinaweza kujiondoa katika muungano huo wakati wowote.

Matukio na matamshi ya hivi majuzi ya viongozi wa chama hicho yanaashiria kuwa, kiko mbioni kuvunja ndoa yake na vyama vingine tanzu vya Azimio.

Jubilee ni kimojawapo cha vyama vitatu vikuu vya Azimio pamoja na ODM na Wiper cha aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka, na Narc Kenya cha aliyekuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Martha Karua.

Viongozi wa Jubilee hawaonekani kuchangamkia masuala ya Azimio huku kiongozi wake Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Muungano huo akijishughulisha na kazi aliyopewa na Rais William Ruto ya kuwa mpatanishi wa amani Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika mkutano wa Ijumaa ambao vinara wa Azimio walikutana na magavana, viongozi wakuu wa Jubilee hawakuhudhuria.Kimya cha Uhuru na kauli za maafisa na wanachama wa Jubilee eneo la Mlima Kenya ikiwemo kumkumbatia Naibu Rais Rigathi Gachagua na kulaumu chama cha ODM kwa hujuma ni baadhi ya dalili kwamba kiko mbioni kubanduka Azimio.

Mnamo Ijumaa, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Bw Kanini Kega, alisema kwamba anamuunga mkono Bw Gachagua kama kiongozi kutoka eneo la Mlima Kenya anayeshikilia wadhifa wa juu zaidi serikalini.

Ingawa alisisitiza angali katika chama cha Jubilee, Bw Kega aliashiria kwamba chama hicho kinawazia kuhama Azimio.

“Niko hapa kama mkurugenzi wa uchaguzi wa Jubilee lakini ikiwa katika siku zijazo tutaweza kufanyia kazi mambo mengine basi itakuwa sawa,” alisema Bw Kega alipokutana na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, mshirika wa Bw Gachagua.

Hatua ya Bw Kega ilijiri siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni kunukuliwa akisema kwamba, chama chao kiko huru kumtema Bw Odinga kwa kuwa walimlipa deni katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Deni ambalo Bw Odinga alitaka alipwe limelipwa. Kwa mara ya kwanza, Odinga alipata kura nyingi za Mlima Kenya ambazo hakuwa amepata na sasa umefika wakati wetu kuondoka,” Bw Kioni alisema.

Mwanasiasa huyo ambaye ni miongoni mwa viongozi wa Jubilee waliojenga Azimio aliashiria kuwa, wanawania zaidi umoja wa Mlima Kenya kuliko kubakia katika upinzani.

“Hali inapobidi, jamii hukimbia kwa haraka na kuungana. Kilicho muhimu ni uaminifu kwa jamii, dalili ziko wazi. Haijalishi kama uko UDA au Kenya Kwanza,” alisema.

Kabla ya matamshi ya Bw Kioni ambayo yaliungwa na aliyekuwa mbunge wa Nyeri Mjini Bw Ngunjiri Wambugu, wabunge wa Jubilee walikuwa wamelaumu chama cha ODM kwa kukiuka mkataba wa muungano wa Azimio baada ya kuondolewa kwa jina la seneta wa Isiolo, Fatuma Dullo katika Tume ya Huduma ya Bunge (PSC).

Kulingana na mkataba wa Azimio, vyama tanzu viko huru kuuhama miezi mitatu baada ya uchaguzi muda ambao tayari umeisha.Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ambaye ni Katibu Mkuu wa ODM alionekana kuharibu mambo kwa kudai kwamba, Jubilee haikutimiza ahadi ya kumpatia Bw Odinga asilimia 40 ya kura ilivyokuwa imeahidi.

“Ni kweli baba (Raila) alipata kura 490,000 zaidi katika Mlima kuliko 2017. Lakini ahadi ilikuwa ni asilimia 40 au kura 2.4 milioni. Jubilee iliahidi makuu lakini haikutimiza yote japo ilisisitiza itoe mgombea mwenza na Gavana wa Nairobi na zaidi ya asilimia 50 ya serikali. Msitubebe,” Bw Sifuna alisema akijibu viongozi wa Jubilee.

Ikihama Azimio, Jubilee itajiunga na Maendeleo Chap Chap, United Democratic Movement (UDM), Pan Afrika Alliance (PAA) na Farmers Party ambavyo vilijiunga na Kenya Kwanza kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

  • Tags

You can share this post!

Mwanariadha Francois Msafiri kutoka DRC alenga kukimbia...

WANTO WARUI: Watahiniwa wanaoanza mitihani yao leo wapewe...

T L