• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:50 AM
Mwanariadha Francois Msafiri kutoka DRC alenga kukimbia 100km kutoka Naivasha hadi Nairobi Jamhuri Dei

Mwanariadha Francois Msafiri kutoka DRC alenga kukimbia 100km kutoka Naivasha hadi Nairobi Jamhuri Dei

Na GEOFFREY ANENE

MTIMKAJI wa mbio za masafa marefu Francois Msafiri ametangaza atakimbia kilomita 100 kutoka mji wa Naivasha hadi ugani Nyayo jijini Nairobi hapo Desemba 12 katika mbio za Jamhuri Day Challenge.

Mkimbizi huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambaye aliwasili Kenya mwaka 2010 akitoroka vita mashariki mwa nchini hiyo, analenga kukamilisha umbali huo kwa saa saba.

Msafiri anadhaminiwa na kocha wake Enock Rotich.

“Bwana Rotich anataka tuonyeshe dunia nzima kuwa tuna uwezo wa kukimbia umbali huo,” alisema mtimkaji huyo ambaye pia ni kinyozi mtaani Syokimau katika kaunti ya Machakos.

Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 26 anasema atatangaza wanariadha watakaomwekea kasi hapo Desemba 5.

“Lengo langu kubwa kukimbia kutoka mjini Naivasha hadi Nyayo ni kusherehekea uhuru kwa Waafrika. Pia, upendo na umoja kwa Waafrika, kusaidiana,” alisema Msafiri hapo Jumapili.

Mtimkaji huyo alikimbia 512km kutoka Mombasa hadi Nairobi mwezi Juni 2021 kwa saa 54 na dakika 27 kuchangisha fedha za kusaidia watoto 5,000 wa wakimbizi nchini kuendeleza masomo yao baada ya janga la virusi vya corona kuvuruga maisha yao.

Mwaka 2022, Msafiri alikimbia 155km kutoka Eldoret hadi Nakuru mwezi Februari kujiandaa kukimbia 320km kutoka Eldoret hadi Nairobi mnamo Juni 3-4.

Mwezi Septemba, Msafiri alifeli katika jaribio lake la kuvunja rekodi ya dunia ya 100km ya raia wa Lithuania Aleksander Sorokin ya saa sita, dakika tano na sekunde 41 alipofanikiwa kukimbia 50km pekee katika shule ya GEMS mjini Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Costa Rica yaduwaza Japan kwa...

Mgawanyiko Azimio ikikaribia kuvunjika

T L