• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Mgombea udiwani wadi ya Kiuu ajipambanua kama kiongozi wa kutatua changamoto za vijana

Mgombea udiwani wadi ya Kiuu ajipambanua kama kiongozi wa kutatua changamoto za vijana

NA SAMMY WAWERU

MGOMBEA wa kiti cha udiwani (MCA) wadi ya Kiuu, Githurai, eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu Bw Oliver Njenga amesisitiza haja ya viongozi kuungana ili kupata suluhu ya changamoto zinazokumba vijana nchini.

Mwaniaji huyo anayemezea mate wadhifa huo kupitia Chama Cha Kazi kinachoongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria amesema ni kupitia ushirikiano ambapo ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana utaweza kuangaziwa.

Akielezea kusikitishwa kwake na ongezeko la visa vya vijana kujitia kitanzi kwa sababu ya mahangaiko wanayopitia, mwanasiasa huyo alisema viongozi wanapaswa kuungana kuanzisha miradi ya maendeleo.

“Majuzi katika wadi ya Kiuu, kuna kijana aliyejitia kitanzi na hata ingawa uchunguzi kubaini kiini cha mkasa huo unaendelea, ugumu wa maisha huenda ukawa ndio ulimchochea kujiondoa uhai,” Bw Njenga akaambia Taifa Leo.

Gharama ya maisha inazidi kuwa ghali, mfumko wa bidhaa za kula ukilemea wananchi.

Mgombea wa udiwani katika wadi ya Kiuu, Githurai, Ruiru, Kaunti ya Kiambu, Bw Oliver Njenga wakati wa mahojiano ambapo aliwahimiza viongozi kushirikiana kuanzisha miradi ya maendeleo kusaidia vijana. PICHA | SAMMY WAWERU

Chini ya kipindi cha muda wa miaka minne, serikali imekuwa ikiongeza bei ya mafuta ya petroli hatua inayoathiri moja kwa moja bidhaa muhimu za kimsingi.

Isitoshe, ushuru wa asilimia nane unaotozwa mafuta unaendelea kutekelezwa, licha ya hali ngumu kiuchumi inayosababishwa na thari za janga la corona.

“Ni kupitia ushirikiano wa viongozi kuanzisha miradi ya maendeleo kubuni nafasi za ajira tutaweza kuangazia shida zilizopo,” Bw Njenga akasema, akihimiza serikali kutathmini ushuru na bei ya bidhaa za kula hasa mafuta, unga, sukari na maziwa.

Mwanasiasa huyo ni mmoja wa waanzilishi wa All Stars Githurai, timu ya soka eneo la Githurai inayokuza vipaji chipukizi katika soka.

“Kwa sababu ya hali ngumu ya maisha, tuwaze na kuwazua jinsi ya kuokoa vijana wetu na kina mama. Tubuni nafasi za kazi kupitia tuktuk na huduma za bodaboda.

“Isitoshe, michezo inalipa, na tunapaswa kuipiga jeki. Watoto wetu na vijana wasome kwa bidii. Ninahimiza kila mmoja wetu, hususan viongozi, ajitokeze tuzindue miradi ya maendeleo,” akafafanua.

Katika wadi ya Kiuu Njenga alidokeza, kwa ushirikiano na wadauhusika wengine, wanaendeleza mpango wa Somo unaowapa fursa kina mama na wasichana, kujifunza kozi mbalimbali kama vile ususi, ufumaji vikapu na pia kuongeza thamani mazao mabichi ya shambani.

You can share this post!

Argentina wacharaza Venezuela katika mechi ya kufuzu kwa...

Jubilee yageuka sumaku kwa wanaolenga ubunge

T L