• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Mikakati ya Kalonzo kurithi Raila Azimio

Mikakati ya Kalonzo kurithi Raila Azimio

NA MOSES NYAMORI

KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka amesuka mikakati ya kurithi ngome za kisiasa za mshirika wake wa miaka mingi, Raila Odinga.

Imefichuliwa kuwa miongoni mwa mipango yake ni kuzuru ngome za Bw Odinga hasa Nyanza na Magharibi kupiga jeki safari yake ya Ikulu 2027.

Bw Musyoka ambaye alimuunga mkono Bw Odinga katika chaguzi za 2013, 2017 na 2022 anataka kutumia hilo kuvuna kura za maeneo ya Nyanza, Magharibi na Pwani, maeneo ambayo yamemuunga mkono Bw Odinga tangu 2007.

Wapanga mikakati wa Bw Musyoka wanaamini Bw Odinga hatawania urais 2027 kwa misingi ya umri na ameanza kumsawiri kiongozi huyo wa Wiper kama sura mpya ya upinzani.

Bw Odinga, 77, atakuwa na umri wa miaka 82 mnamo 2027 Wakenya watakapoelekea debeni kuwachagua viongozi wapya.

Ni kwa msingi huu ambapo Bw Musyoka amekataa pendekezo la Rais William Ruto kwamba, ajiunge na serikali ya muungano wa Kenya Kwanza (KKA).

Baadhi ya wandani wake waliambia Taifa Jumapili kwamba, Bw Musyoka ameratibu ziara kadha katika maeneo yaliyounga mkono muungano wa Azimio katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kuwashukuru wafuasi wao.

Juzi, kiongozi huyo wa Wiper aliongoza mkutano uliowaleta pamoja makatibu wakuu wa vyama tanzu katika Azimio jijini, Nairobi, bila kuwepo kwa Bw Odinga.

Baadaye, alitoa taarifa akimsuta Rais Ruto kwa kulenga maafisa wa Kitengo cha Upelelezi wa Uhalifu (DCI) kutokana na sababu za kisiasa.

Aidha, amekuwa akitoa taarifa za kukosoa utawala wa Dkt Ruto kuhusiana na kupanda kwa gharama ya maisha na bei ya mafuta.

Mnamo Oktoba 22, Bw Musyoka alizuru Homa Bay kuhudhuria mazishi ya babake Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma.

Kiongozi huyo alilakiwa vizuri na Gavana Gladys Wanga pamoja na viongozi wa eneo hilo la Luo Nyanza.

Siku iliyofuata, Bw Musyoka alitua mjini Kisumu kuhudhuria ibada ya Jumapili ambapo aliandamana na viongozi wa Azimio kutoka eneo hilo.

Miongoni mwao walikuwa magavana; Anyang’ Nyong’o (Kisumu), James Orengo (Siaya), Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’, Ruth Odinga (Mbunge Mwakilishi wa Kike), Antony Oluoch (Mbunge wa Mathare), miongoni mwa wengine.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Bw Musyoka alifichua kuwa ataanza kampeni yake ya urais ya 2027 baada ya uchaguzi huo.

Alisema angeiga Dkt Ruto ambaye alianza kampeni ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta muda mfupi baada ya wao kuanza muhula wao wa pili 2017.

“Naibu Rais Ruto (sasa Rais) alianza kampeni baada ya kuchaguliwa kwao tena mnamo 2017 kwa sababu alijua kuwa analenga urais,” Bw Musyoka akasema mnamo Machi 2022.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi anasema ngome ya Bw Odinga inamkubali Bw Musyoka kwa sababu amemuunga mkono katika chaguzi tatu zilizopita.

Anasema kiongozi huyo wa Wiper yu huru kuzuru sehemu yoyote katika eneo la Nyanza kwa sababu “hapa ni nyumbani”.

You can share this post!

Maseneta watishia kuzima CDF

Serikali sasa yapata Sh25b kukabili njaa

T L