• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Mkataba sasa waanika unafiki wa Naibu Rais

Mkataba sasa waanika unafiki wa Naibu Rais

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto anapanga kuingilia uhuru wa Idara ya Mahakama kwa kugawa nyadhifa katika idara hiyo endapo atachaguliwa kuwa rais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kwa mujibu wa mkataba wa ugavi wa mamlaka kati ya vyama vitatu vikuu ndani ya muungano wa Kenya Kwanza (KKA), vyama vitapata asilimia 60 ya nafasi katika vitengo vya Serikali Kuu, Idara ya Mahakama na Bunge.

Kulingana na mkataba huo, ambao uliwasilishwa katika afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu Jumapili, chama cha United Demcratic Alliance (UDA) kitapata asilimia 30 ya vyeo katika vitengo hivyo vya serikali, vyama vya ANC na Ford Kenya vikipata asilimia 30 huku vyama vingine vidogo vikigawana asilimia 40 zilizosalia.

Aidha, mnamo Aprili 22, 2022 kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi aliuambia mkutano wa hadhara kwamba kando na kugawana nyadhifa katika nguzo hizo tatu za serikali, KKA pia itagawana nyadhifa za ubalozi na mashirika ya serikali kwa mfumo huo huo (asilimia 30:30: 40).

“Katika mpango huu, jamii ya Waluhya itapata asilimia 30 ya nafasi za uwaziri, asilimia 30 ya teuzi katika idara ya mahakama na asilimia 30 ya vyeo vya ubalozi,” Bw Mudavadi akasema katika Chuo cha Mafunzo ya Biblia cha Nyang’ori.

Lakini wadadisi wa masuala ya sheria na uongozi wanasema kuwa ni kinyume cha Katiba ya sasa kwa Dkt Ruto na wenzake katika muungano wa KKA kupanga kugawanya nyadhifa katika idara ya mahakama.

“Uhuru wa Idara ya Mahakama unalindwa na Katiba ya sasa na Rais wa nchi hawezi kuingilia uhuru huo kwa njia yoyote ile ikiwemo ugavi wa nyadhifa. Teuzi za majaji na maafisa wengine wa idara ya mahakama huendeshwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) wala si Afisi ya Rais,” akasema Bw James Mwamu ambaye ni wakili.

“Ni uhuru huu ambao umewezesha idara hiyo kutoa maamuzi yanayokinzana na misimamo ya serikali katika miaka ya hivi karibuni,” akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu Jumatatu huku akipuuzilia mbali mpango wa Kenya Kwanza kugawana mamlaka ya idara ya mahakama.

Vile vile, kipengele cha 172 cha Katiba, kinasema kuwa JSC itadumisha “uhuru na uwajibikaji wa idara ya mahakama inapoendesha shughuli zake kuhakikisha uwepo wa haki na uwazi katika usimamizi wa mfumo wa utekelezaji wa haki”.

Mpango wa Dkt Ruto na wenzake wa “kugawana idara ya mahakama” ni kinyume na msimamo wake wa awali wa kutetea uhuru wa idara hiyo.

BBI

Alipokuwa akiendesha kampeni ya kupinga mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) mnamo 2020, Dkt Ruto alipinga pendekezo la kuanzishwa kwa afisi ya kuchunguza utendakazi wa majaji (Ombudsman).

Alisema kuwa pendekezo kwenye mswada wa BBI kwamba afisa huyo atateuliwa na Rais, halikufaa kwani hiyo ilikuwa ni sawa na kuhujumiwa kwa uhuru wa idara ya mahakama.

“Tunapinga kabisa pendekezo la kuwepo kwa ‘ombudsman’ ambaye atateuliwa na Rais kwa hii ni sawa na kuingilia idara ya mahakama. Uhuru wa sasa hii unafaa kulindwa kwa sababu ndio kimbilio la wanyonge. Tunasema hivyo kwa kuwa hatutaki kurejea katika enzi ambapo majaji walipokea simu kutoka kwa wakuu fulani, baada ya mikutano kufanyika usiku. Hatutaki kurejea huko,” Dkt Ruto akasema kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini Aprili 22, 2021.

Aidha, Naibu Rais na wandani wake wamekuwa wakishikilia kuwa muungano wao haongozwi na falsafa ya ugavi wa nyadhifa bali haja ya kuinua maisha ya walalahoi.

“Serikali ambayo itaundwa na UDA pamoja na marafiki zetu katika Kenya Kwanza ni ile ambayo mama mboga na wanabodaboda ndio watakuwa na usemi mkubwa. Mahalsa ndio watapewa nafasi ya kujiinua kiuchumi na kibiashara,” Dkt Ruto akasema.

“Sisi sio kama wale washindani wetu katika Azimio ambao haja yao kuu ni kubadilisha Katiba ili kuunda vyeo kwa viongozi matajiri. Lengo lao kuu ni kugawana mamlaka miongoni mwao na hawajali masilahi ya watu hawa wadogo,” akaongeza alipoidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais wa UDA katika uwanja wa Kasarani, mwezi Aprili.

  • Tags

You can share this post!

Washirika Azimio wakaba Raila koo

Veemisc ni mwanamuziki anayefanya vizuri pia katika...

T L