• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Washirika Azimio wakaba Raila koo

Washirika Azimio wakaba Raila koo

NA LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga anaonekana kukabwa koo na washirika wake, hali ambayo imeanza kuzua misukosuko ndani ya muungano huo wenye vyama 26.

Wadadisi wa siasa wanasema Bw Odinga tayari ameonyesha dalili za kutokuwa na usemi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo uteuzi wa mgombea mwenza wake, huku washirika tofauti wakivutia kwao.

“Ukweli ni kwamba mwaniaji mwenza atakuwa chaguo la Uhuru. Hata kama Bw Odinga hamtaki atalazimika kumkubali. Bw Odinga kwa sasa ni mateka kwani anahitaji Uhuru kwa hali na mali. Uhuru akikataa kumuunga mkono leo, ndoto yake ya kuingia Ikulu itasambaratika,” anasema mdadisi Javan Bigambo.

Msomi wa sheria Prof Medo Misama anakubaliana na Bw Bigambo kuwa Bw Odinga hana budi kukubali mwaniaji mwenza atakayepewa na Rais Kenyatta.

“Mwaniaji wa ugavana wa Nairobi Polycarp Igathe aliletwa na Rais Kenyatta licha ya Bw Odinga kuwa na mgombea wake Bw Tim Wanyonyi. Ilibidi Bw Odinga asalimu amri na kumwondoa Bw Wanyonyi. Hiyo ni ishara kwamba Rais Kenyatta ndiye mwenye usemi ndani ya Azimio wala si Bw Odinga,” anasema Prof Medo.

Huku wandani wa Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka wakisisitiza kuwa ni sharti ateuliwe mwaniaji mwenza wa Raila, wale wa Rais Uhuru Kenyatta wameshikilia kuwa wadhifa huo umetengewa chama cha Jubilee.

Wabunge Nduati Ngugi (Gatanga) na Peter Kimari (Mathioya) Jumatatu waliambia Taifa Leo kuwa Jubilee ndicho chama chenye usemi kuhusu mwaniaji mwenza.

“Azimio ina washirika wakuu watatu ambao ni ODM, Jubilee na One Kenya Alliance. Haiwezekani kwa Jubilee kupuuzwa. Sisi ndio tutatoa mwaniaji mwenza,” akasema Bw Ngugi.

Wapwani nao wanasisitiza ni sharti wakati huu mgombea mwenza wa Bw Odinga awe ni kutoka eneo hilo, huku washirika wengine katika Azimio wakisukuma Martha Karua wa Narc-Kenya.

Wadadisi wanaonya kuwa Rais Kenyatta na Bw Odinga wasipocheza vyema karata ya kuteua mwaniaji mwenza huenda muungano huo ukapoteza washirika wengi.

“Bw Musyoka akiteuliwa kuwa mwaniaji mwenza, Bw Odinga atakuwa na hakika ya kuzoa karibu kura zote milioni 2 za Ukambani. Lakini changamoto iliyopo ni kwamba Kalonzo hatatetea masilahi ya watu wa eneo la Mlima Kenya. Raila ana kibarua kigumu sana cha kuridhisha washirika wake walio na maslahi tofauti,” asema Bw Bigambo.

Suala lingine ambalo linamkoroga Bw Odinga ni madai ya vyama vidogo kuwa vinadhulumiwa ndani ya muungano wa Azimio.

Jana Jumatatu, Gavana wa Machakos Alfred Mutua na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi walitangaza kuhama Azimio na kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Chama cha Bw Kingi cha Pamoja African Alliance (PAA) kilisema kimejiondoa kwa kunyanyaswa na ODM katika maeneo ya Pwani, haswa Kaunti ya Kilifi.

Gavana Kingi pia analalamikia kutengwa katika kampeni za Azimio katika eneo la Pwani.

Chama cha Uzalendo (CCU) chake aliyekuwa Mkuu wa Wafanyakazi wa Ikulu, Nzioka Waita pia kimetishia kutoroka Azimio.

Vyama vy CCU, PAA na Maendeleo Chap Chap viliingia Azimio kupitia Jubilee ambapo viliteua Rais Kenyatta kuwa mtetezi na msemaji wao katika Azimio.

“Vyama vingi viliingia ndani ya Azimio kupitia kwa Rais Kenyatta, hivyo ni yeye tu anayefaa kushughulikia malalamishi ya viongozi wavyo. Kusalia kimya kwa rais huku vyama vikijiondoa katika muungano huo ni pigo kwa Bw Odinga,” anasema Prof Misama.

Bw Odinga pia anakabiliwa na changamoto ya vyama washirika kudhamini wagombeaji katika maeneo sawa, kuu ikiwa ni Mombasa ambapo kuna Abdulswamad Nassir wa ODM na Mike Sonko wa Wiper.

Jijini Nairobi Wiper pia kimesema kitadhamini wagombeaji kumenyana na wale wa ODM na Jubilee.

Katika Kaunti ya Kajiado, ODM kinaunga mkono Gavana Joseph Ole Lenku huku Jubilee ikisimamisha gavana wa zamani David ole Nkedianye.

Katika Kaunti ya Kisii, muungano huo umesimamisha Sam Ongeri wa DAP-K na Simba Arati (ODM).

  • Tags

You can share this post!

Mabingwa wa tenisi Afrika Mashariki U-14 Kenya warejea...

Mkataba sasa waanika unafiki wa Naibu Rais

T L