• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Mpango fiche wa Ruto kuzamisha jahazi la Azimio

Mpango fiche wa Ruto kuzamisha jahazi la Azimio

ONYANGO K’ONYANGO Na RUTH MBULA

RAIS William Ruto ameanzisha mikakati ya kusambaratisha muungano wa Azimio na kumaliza ushawishi wa viongozi wake.

Rais anaonekana kuendeleza mikakati ya kumvuruga na kumlemaza kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga kwa kupenya katika ngome za mwanasiasa huyo mkongwe.

Katika siku za hivi karibuni Dkt Ruto amefanya msururu wa mikutano katika Ikulu ya Nairobi na wanasiasa wakuu kutoka ngome za Bw Odinga za Gusii na Magharibi ya Kenya.

Wiki jana, Rais Ruto alikutana na jumbe za viongozi kutoka maeneo hayo mawili kwa mazungumzo ambayo yalidaiwa kujikita katika ajenda za maendeleo kufaa wakazi.

Aidha, duru zinasema kuwa kuna mipango ya kiongozi wa taifa kukutana na viongozi wengine, wakiwemo wale wa Azimio, kutoka maeneo ya Pwani, Ukambani na Luo Nyanza.

Kwa mfano, jana Jumapili Gavana wa zamani wa Nairobi Evans Kidero ni miongoni mwa viongozi walioandamana na Rais Ruto kwenye hafla ya maombi ya kutoa shukrani katika Chuo Kikuu cha Embu.

Bw Kidero, ni miongoni mwa viongozi wakosoaji wakuu wa Bw Odinga kutoka Luo Nyanza.

Wadadisi wanabashiri mikutano hiyo kuwa mbinu ya Rais Ruto kupenya kisiasa katika ngome hizo za Bw Odinga mbali na kuiwezesha serikali yake kukubalika hata katika maeneo ambako hakupata kura nyingi uchaguzi uliopita.

Mnamo Ijumaa wiki jana, kabla ya kuondoka nchini kwa ziara ya siku moja nchini Sudan Kusini, Dkt Ruto alikutana na viongozi kutoka ene la Gusii.

Ujumbe huo ulioongozwa na Gavana wa Kisii Simba Arati na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.

Gavana Arati amekuwa mwandani wa Bw Odinga kwa miaka mingi tangu enzi zake akihudumu kama diwani maalum wa ODM katika lililokuwa Baraza la Jiji la Nairobi kisha akawa mbunge wa Dagoreti Kaskazini kwa mihula miwili hadi Agosti mwaka huu.

Kabla ya mkutano wa Ijumaa, Rais Ruto alikutana na Bw Arati Jumamosi iliyotangulia ambapo aliahidi kufanya kazi na jamii ya Abagusi katika nyanja za maendeleo.

Eneo la Gusii lilimpigia Odinga kura kwa wingi katika uchaguzi uliopita na sasa jamii inaonyesha dalili za kujitenga na Azimio na kusogea karibu na mrengo wa United Democratic Alliance (UDA) katika muungano wa Kenya Kwanza.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa urais, Bw Odinga alipata asilimia 65.80 za kura katika kaunti ya Kisii.

Katika kaunti ya Nyamira kiongozi huyo wa Azimio alipata asilimia 61.84 ya kura.

Alhamisi Rais Ruto pia alikuwa na ujumbe kutoka Magharibi ya Kenya wakiongozwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli.

Japo, viongozi hao walidai kuwa ajenda kuu katika mkutano huo ilikuwa maendeleo inaaminika kuwa siasa ndizo zilipewa kipaumbele.

Ndiposa akihutubu katika hafla ya mazishi kijiji Ebuchero, eneo bunge la Khwisero, kaunti ya Kakamega, Bw Atwoli alibashiri kuwa Dkt Ruto atashinda kwa urahisi katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Sikuamini Ruto angeshinda katika uchaguzi. Lakini huyu kijana ni mwerevu na alikuwa amejipanga vilivyo. Ikiwa alitupiga chenga serikali ikiwa upande wetu, sasa nini kitamzuia kupata ushindi mkubwa 2027?” Atwoli akauliza.

Katibu huyo mkuu wa COTU amekuwa mwandani wa karibu wa Bw Odinga na aliongoza kampeni za kumpuuzilia mbali Dkt Ruto akimtaja kama “kiongozi asiyefaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta”.

Kulingana na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi XN Iraki, Rais anakutana na viongozi mbalimbali kwa lengo la kujiongezea mamlaka jinsi Hayati Daniel Moi alikuwa akifanya.

“Anajaribu kusambaza ushawishi wake, kwa kuhakikisha kuwa mayai yote ya kisiasa hayako katika kikapu kimoja huku akilenga uchaguzi mkuu wa 2027. Hii ndio maana anatumia mamlaka ya afisini yake kuwavutia wandani wa Odinga upande wake. Ameanza mapema baada ya kung’amua kuwa hiyo ndio mbinu iliyomsaidia kushinda katika uchaguzi uliopita,” anaongeza Profesa Iraki.

  • Tags

You can share this post!

Raila ataja sababu za kumkabili Ruto

TAHARIRI: Bajeti za kaunti zizingatie pia maoni ya umma

T L