• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
Raila ataja sababu za kumkabili Ruto

Raila ataja sababu za kumkabili Ruto

NA JUSTUS OCHIENG’

KINARA wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga jana Jumapili alielezea mambo sita yanayomfanya kukosana na Rais William Ruto.

Bw Odinga aliyekuwa akizungumza alipokuwa akimpigia debe mwaniaji wa udiwani wa Jubilee, Patrick Karani, katika Wadi ya Utawala, Nairobi, aliwataka wafuasi wake kujiandaa kwa ajili ya ‘mapambano makali’ dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.

Waziri huyo mkuu wa zamani aliwataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi Jumatano katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi.

Bw Odinga ataandaa mkutano mwingine katika uwanja huo Desemba 12 wakati wa sherehe za Jamhuri.

Bw Odinga aliorodhesha mambo sita yanayomfanya kukosana na Rais Ruto.

Alisema mambo yanayomkosanisha na Dkt Ruto ni kupanda kwa gharama ya maisha, hatua ya serikali kuhangaisha makamishna wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kutimua watumishi wa umma kiholela wakiwemo Makatibu wa Wizara waliokuwa wameteuliwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Malalamishi mengine ya Bw Odinga dhidi ya Rais ni hatua ya serikali kukosa kutoa mikopo ya Hustler Fund isiyokuwa na riba kama alivyoahidi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, ‘kupendelea’ baadhi ya jamii katika uteuzi serikalini na mpango wa kuagiza magunia milioni 10 ya mahindi yaliyobadilishwa vinasaba GMO) kutoka ughaibuni.

Kigogo huyo wa siasa za upinzani alisema kuwa kama Azimio la Umoja, washafanya ukaguzi kuhusu uchaguzi mkuu uliopita na atawaeleza Wakenya jinsi kura zao zilivyoibwa.

“Tumefanya utafiti wa kutosha na tunajua jinsi kura zetu zilivyoibwa na ngapi walituibia. Tutasema siku ya Jumatano,” akasema Bw Odinga.

Alikuwa ameandamana na mbunge wa Embakasi Mashariki, Bw Babu Owino, Seneta wa Vihiga, Bw Godfrey Osotsi, Bw Karani pamoja na madiwani wa Kaunti ya Nairobi.

Katika mkutano huo, Bw Odinga alimkashifu mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akidai kuwa alihusika katika kuiba kura zake na akawataka Wakenya wafike Kamkunji Jumatano kwa wingi ili wasikilize mwelekeo atakaoutoa.

“Gharama ya maisha imepanda maradufu, na Ruto amekataa kurejesha bei ya pakiti ya unga wa kilo mbili kutoka Sh200 hadi Sh70 jinsi alivyodai wakati wa kampeni. Sasa anawataka Wakenya wasubiri mwaka mzima. Tulipokuwa tukitoa ahadi, tulifahamu mahali ambapo pesa zingetoka. Ni wazi kuwa watu hawa hawakuwa na uhakika kuwa watakuwa rais hadi pale Chebukati alipowasaidia. Lazima wawajibikie Wakenya kuhusu ahadi walizotoa,” akaongeza Bw Odinga akionekana mwingi wa hasira.

Kiongozi huyo wa ODM alisisitiza kuwa hatakaa kitako na kutazama serikali ya Dkt Ruto “ikiwarejesha Wakenya katika enzi za giza” katika kile kilichoonekana kama mwanzo wa wingu la maasi dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.

Rais Ruto na Bw Odinga wameonekana kurushiana cheche kali katika majuma mawili yaliyopita hasa kuhusu hatima ya makamishina wanne wa IEBC.

Uhasama kama huo kati ya viongozi hao wawili wakuu ulishuhudiwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Tofauti zao zimeenea hadi mtandaoni kwa kuwa mnamo Jumamosi, Rais Ruto alitumia ukurasa wake wa twitter kumkashifu Bw Odinga kwa kutishia utawala wake kupitia maandamano baada ya kukosa urais.

“Hata kwa ushirikiano na serikali bado ulipoteza uchaguzi. Koma kujidanganya na kujihadaa,” Rais aliandika.

Hatima ya makamishina hao itaamuliwa na jopo,” akaandika Rais Ruto akirejelea jopo alilounda kuwachunguza makamishina hao wanne ambalo ripoti yake itaamua hatima yao.

Tayari Rais Ruto alikuwa amewasimamisha kazi makamishina hao ila Bw Odinga alisema kuwa kiongozi wa nchi amebadilisha msimamo wake akitumia kanda ya video ya mnamo 2007.

Wakati huo huo, Rais Ruto ameonya Bw Odinga dhidi ya kuvuruga ajenda za serikali yake kupitia maandamano kote nchini.

“Wanajua kuwa tuko na mipango kwa watu wetu na ndio maana wanataka kuleta fujo ili kuvuruga mipango yetu. Lakini ningetaka kuwaambia kwamba mwaka huu na wakati huu watajua hawajui!” Dkt Ruto akasema.

“Tunataka kuendeleza taifa hili na hautaturudisha nyuma,” akaongeza.

Rais Ruto alisema amemshauri Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kushirikiana na wapanga mikakati wa Odinga ili apate ratiba yao ya maandamano kusudi wapewe usalama wa kutosha.

“Nimemshauri Waziri Kindiki aongea nao na wampe ratiba yao ndiposa wapewe usalama wasije wakaharibu mali ya Wakenya. Wanafaa kubaini kama wanataka kufanya maandamano kila siku, kila wiki, kila mwezi au kwa miaka mingapi” Dkt Ruto akasema.

Sababu za Raila kumkabili Ruto

1. Gharama ya juu ya maisha
2. Kuhangaisha makamishna wanne wa IEBC
3. Kutimua watumishi wa umma kiholela wakiwemo Makatibu wa Wizara wa Uhuru
4. Kukosa kutoa mikopo ya Hustler Fund isiyokuwa na riba
5. Kubagua baadhi ya jamii katika uteuzi serikalini
6. Mpango wa kuagiza mahindi ya GMO
  • Tags

You can share this post!

Serikali kuyakagua mahindi yaliyo melini kuhakikisha ni...

Mpango fiche wa Ruto kuzamisha jahazi la Azimio

T L