• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:26 PM
Msipeleke tamaa bungeni, Raila aonya viongozi

Msipeleke tamaa bungeni, Raila aonya viongozi

NA WINNIE ONYANDO

KINARA wa ODM, Raila Odinga amewaonya wabunge wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya dhidi ya kuonyesha ubinafsi na kupigania nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Rais William Ruto.

Akizungumza Ijumaa baada ya kukutana na wabunge wa muungano huo Kaunti ya Machakos, Bw Odinga aliwataka wabunge wake waungane na kutumia idadi yao bungeni kuleta mabadiliko nchini.

Alisema kuwa muungano huo unawategemea wabunge hao hasa katika kuleta mabadiliko katika mahakama ya upeo na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC).

“Msipigane vita miongoni mwenu. Tuko katika muungano wa Azimio na kila mmoja anafaa kufahamu kuwa sote ni kitu kimoja. Usipoteuliwa katika wadhifa fulani, usimchukie mwenzako. Tuungane ili pamoja tusonge mbele,” akasema Bw Odinga.

“Kikao hiki kiliandaliwa ili kuwaunganisha wajumbe wetu na kuwahimiza walinde maslahi yetu kama muungano bungeni. Msipoungana, basi mtatawaliwa bungeni,” akaongeza Bw Odinga.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga alidai kuwa kando na muungano huo kuibiwa katika kura za ngazi ya urais, wana ushahidi kuwa wagombeaji wa Azimio pia waliibiwa katika ngazi za chini.

“Katika ngazi za chini, ninaamini kwamba watu wetu waliibiwa ili kupisha njia kwa wagombea wa UDA,” akasema Bw Odinga.

Kiongozi huyo pia alishutumu hatua ya Rais Ruto kuwaapisha majaji akidai ni njia mojawapo wa kuhonga mahakama na kuifanya kukosa uhuru wake.

“Kuna njama ya kuihonga mahakama. Hii ndio maana Rais alifanya hima kuwaapisha majaji na hata kutengea mahakama pesa,” akasema Bw Odinga.

Alisema kuwa jukumu la wabunge litakuwa kutekeleza majukumu matatu.

“Bunge linafaa kuiokoa idara ya Mahakama ambayo imetekwa nyara na serikali tawala, kubadilisha tume ya IEBC na kuwaokoa wananchi dhidi ya uongozi mbaya,” akasema Bw Odinga.

“Bunge lazima lisimame dhabiti na kuvilinda vyama vyetu vya kisiasa. Tuna jukumu kama Azimio kuchukua madaraka na kutumia idadi yetu Bunge kuhakikisha kuwa wananchi wanatumikiwa ipasavyo.”

Kwa upande wake, kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua aliwahimiza wabunge wa Azimio kuungana ili kuepuka kutawaliwa na mrengo wa Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Muungano wa Kenya Kwanza waibuka na wawaniaji wake wa...

Wauguzi waongeza ujuzi kupitia mpango wa ushirikiano wa...

T L