• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:50 AM
Mudavadi asisitiza NASA iko kwenye chumba mahututi cha kisiasa

Mudavadi asisitiza NASA iko kwenye chumba mahututi cha kisiasa

Na SAMMY WAWERU

NATIONAL Super Alliance (NASA) iko kwenye chumba mahututi cha kisiasa, amesema kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi.

Muungano wa Nasa ulibuniwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, ambapo kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga alipeperusha bendera yake kuwania urais.

Mgombea mwenza alikuwa Bw Kalonzo Musyoka (Wiper).

Aidha, Mudavadi ndiye alikuwa mwasisi wa muungano huo ila sasa anasema umesambaratika. “Kiafya, Nasa haipo kwenye hali njema,” akasema.

Mbali na Mabw Odinga, Mudavadi na Kalonzo, Seneta Moses Wetangula (Ford-Kenya) na aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Rutto (Chama Cha Mashinani) pia walikuwa miongoni mwa vinara wa Nasa.

Bw Mudavadi amefichua kwamba kilichochangia mgawanyiko katika muungano huo ni ukosefu wa uaminifu.

“Tulitia saini mkataba wa makubaliano (MoU) ODM iwasilishe mgombea wa urais 2017, kisha katika chaguzi zitakazofuata vyama vingine viruhusiwe. Tunavyoona, mkataba huo umekiukwa,” akasema.

“Kisheria Nasa ipo ila kimaafikiano haipo,” Bw Mudavadi akaelezea.

Kiongozi huyo wa ANC pia alisema makubaliano yaliyokuwepo kuhusu mgao wa fedha za vyama, umekiukwa, akisisitiza kwamba ukosefu wa uaminifu umesababisha kusambaratika kwa muungano huo.

“Tulipaswa kuwa tukigawana fedha za Nasa kwa mujibu wa vyama, hilo halipo,” akasema.

Katika siku za hivi karibuni, Bw Mudavadi na Kalonzo wamekuwa wakimhimiza kiongozi wa ODM Raila Odinga kuunga azma yao kuingia Ikulu 2022.

Bw Odinga hata hivyo ameweka wazi kwamba hataunga kiongozi yeyote mkono, hatima yake kuwania urais mwaka ujao ikiwa ingali kitendawili.

You can share this post!

Mradi wa ujenzi wa kituo cha elimu na mafunzo kukabiliana...

Leeds United yapepeta Southampton 3-0 katika EPL