• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Mudavadi kujua majukumu yake baada ya siku 30

Mudavadi kujua majukumu yake baada ya siku 30

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi atalazimika kusubiri kwa zaidi ya siku 30 kabla ya kupewa majukumu ya afisi ya Mkuu wa Mawaziri katika serikali ya Jubilee.

Duru zimearifu Taifa Leo kwamba baada ya kuapishwa kesho Jumanne, Rais Mteule William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua watafanya mkutano wa faragha Jumatano kuteua baraza la mawaziri.

Kulingana na Katiba ya sasa, Rais anaruhusiwa kuteua mawaziri wasiopungua 14 na wasiozidi 22.

Kwa kuwa wadhifa wa Mkuu wa Mawaziri (Waziri Mkuu) hautambuliwi na Katiba ya sasa, Dkt Ruto atalazimika kubuni wadhifa huo kwa kudhamini mswada bungeni.

Hii ndiyo maana kwa mujibu wa mkataba uliobuni muungano wa Kenya Kwanza, muungano huo utawasilisha mswada katika bunge ambao utafafanua majukumu ya afisi hiyo.

“Mswada huo ambao utawasilishwa bungeni, utalenga kuifanyia marekebisho Sheria ya Ushirikishi wa Majukumu ya Serikali ya Kitaifa ya 2013 ili kujumuisha afisi ya Mkuu wa Mawaziri na kuelezea majukumu yake,” mkataba huo unasema.

Kulingana na mkataba huo, ambao uliwasilishwa kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu, Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula aliahidiwa kiti cha uspika wa Bunge la Kitaifa, Kenya Kwanza ikishinda kiti cha urais.

Uspika

Naye, aliyekuwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi aliahidiwa wadhifa wa uspika wa Seneti.

Dkt Ruto amefanikisha kutekelezwa kwa ahadi iliyotolewa kwa Mbw Wetang’ula na Kingi kwani mnamo Alhamisi walichaguliwa kwa urahisi kuongoza mabunge hayo mawili.

Alifanya hivyo kwa kuwashawishi baadhi ya wabunge wa Azimio la Umoja One Kenya na wabunge huru kuwapigia kura wawili hao katika uchaguzi ulioendeshwa katika mabunge hayo mawili.

Shughuli hiyo iliendeshwa baada ya kuapishwa kwa wabunge 349 na maseneta 66, katika vikao vilivyoongozwa na makarani wa mabunge hayo.

Afisa mmoja wa cheo cha juu katika chama United Democratic Alliance (UDA) Ijumaa aliambia Taifa Leo kwamba Dkt Ruto atamtunuku Bw Mudavadi wadhifa wa uwaziri katika Wizara moja yenye “ushawishi mkubwa kabla ya kupitishwa kwa sheria ya kutoa majukumu ya Afisi ya Mkuu wa Mawaziri”.

Hata hivyo, akiongea katika mkutano wa kampeni katika eneobunge lake la Sabatia mnamo Julai 29, Bw Mudavadi alidokeza kuwa baadhi ya majukumu ya afisi yake yatakuwa kusimamia na kushirikisha majukumu ya wizara zote za serikali.

“Katika serikali ya Kenya Kwanza, nitashikilia cheo cha Mkuu wa Mawaziri, ambacho sasa kinasimamiwa na Waziri Fred Matiang’i,” akasema.

Hata hivyo, Dkt Ruto mwenyewe aliahidi kuwa baada ya kuapishwa kwake atatia saini Agizo la Rais ambalo litafafanua majukumu ya afisi za Naibu Rais, Mkuu wa Mawaziri, Mawaziri na maafisa wengine wa serikali.

  • Tags

You can share this post!

Mvurya mwenye imani tele Kingi atalinda ugatuzi

Mwaniaji wa UDA sasa ataka kura za Mvita zihesabiwe upya

T L