• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Mwaniaji wa UDA sasa ataka kura za Mvita zihesabiwe upya

Mwaniaji wa UDA sasa ataka kura za Mvita zihesabiwe upya

NA BRIAN OCHARO

ALIYEKUWA mgombeaji ubunge Mvita kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Omar Shallo, anataka mahakama iagize kura zihesabiwe upya kama njia mojawapo ya kuthibitisha uchaguzi huo haukukumbwa na dosari.

Bw Shallo ameelekea mahakamani kupinga ushindi wa Bw Mohamed Machele, mwanachama wa ODM, akidai kwamba uchaguzi ulikumbwa na wizi wa kura, ghasia, utepetevu wa maafisa wa uchaguzi na utoaji rushwa kwa wapigakura.

Kuhusu wizi wa kura, Bw Shallo amedai kuwa kura ziliongezwa katika baadhi ya vituo na kuathiri matokeo yaliyotangazwa.

Amedai kuwa, katika kituo cha 2 cha Allidina Visram, jumla ya wapigakura waliojiandikisha walikuwa 690 ilhali jumla ya kura zilizopigwa ni 1,369.

Bw Shallo ameomba kwamba kwa kuzingatia hitilafu katika kituo cha 2 cha Allidina Visram, na matukio ya ghasia, haitakuwa rahisi kwa mahakama kutoa uamuzi kwa uadilifu kuhusu hitilafu hizo bila kufanya uchunguzi wa masanduku ya kura.

Pia, mlalamishi huyo amewashutumu wasimamizi wa uchaguzi kwa utovu wa nidhamu kwa madai kuwa walijaza fomu za kutangaza matokeo katika kituo cha kujumlishia kura bila kuwepo kwa mawakala wa wagombea au vyama vya siasa.

Zaidi ya hayo, anadai kuwa uchaguzi haukuzingatia matakwa ya wapigakura.

Katika uchaguzi huo, Bw Machele alitangazwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) baada ya kupata kura 22,611 huku Bw Shallo akiibuka wa pili kwa kupata kura 11,125.

Mlalamishi huyo pia anadai kuwa baadhi ya vituo vilifunguliwa kwa kuchelewa lakini IEBC haikuongeza muda wa kupiga kura.

Kwa mujibu wa Bw Shallo, maeneo ambayo yalichelewa kufunguliwa yalizua sintofahamu kwa wapigakura ambao walijitokeza mapema saa kumi na moja asubuhi kupiga kura.

Kuhusu utoaji hongo, alidai kuwa mpinzani wake aliwahonga wapigakura Sh1,000 ili kumchagua.

Mlalamishi huyo pia anadai wahalifu ambao walikuwa na mavazi ya kijeshi walitumiwa kuwatishia wapigakura kwa vurugu na kuwanyima nafasi ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Vilevile, amedai kuwa IEBC ilifanya uchaguzi kinyume cha sheria katika vituo ambavyo havijachapishwa.

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi kujua majukumu yake baada ya siku 30

Ruto asikie kilio cha Wakenya – Elachi

T L