• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mvutano Bondeni wanasiasa wakiweka harakati za kugawana viti

Mvutano Bondeni wanasiasa wakiweka harakati za kugawana viti

Na BARNABAS BII

PENDEKEZO kwamba nyadhifa za kisiasa zigawanywe kwa msingi wa kikabila hasa katika kaunti za Kaskazini mwa Bonde la Ufa, limezua mgawanyiko miongoni mwa wanasiasa uchaguzi mkuu ukitarajiwa mwaka 2022.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipendekeza nafasi za uongozi zigawanywe ili watu asili wa eneo na makabila mengine yanufaike katika kaunti zenye jamii mbalimbali katika kaunti za Uasin Gishu, Trans-Nzoia na Elgeyo-Marakwet.

Hata hivyo, pendekezo hilo la baadhi ya wazee wa jamii ya Kalenjin, limepingwa na wapigakura ambao wanataka washindi wa nyadhifa za uongozi wapatikane debeni.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu kuna uhasama mkubwa kati ya jamii ya Nandi na Keiyo kuhusu hasa nani anafaa kurithi kiti cha ugavana baada ya Jackson Mandago kumaliza muhula wake wa pili.

Hii ni baada ya jamii hizo kuelewana 2013, kuwa Bw Mandago (Nandi) apokezwe ugavana kisha Naibu wake Daniel Chemno awe kutoka Keiyo, makubaliano ambayo yalidumishwa hata katika kura ya 2017.

Mnamo 2022, jamii ya Keiyo sasa inatarajia wenzao wa Nandi ‘kurudisha mkono’ na kumuunga mmoja kutoka jamii yao kutwaa ugavana hasa kupitia UDA ambacho ni maarufu eneo hilo kwa kuwa kinavumishwa na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany, anayelenga kiti cha ugavana na mbunge wa Kapsaret, Bw Oscar Sudi, wametofautiana kuhusu suala hilo huku Bw Kositany akisisitiza kuwa anayetaka ugavana lazima aungwe mkono na jamii ya Nandi.

Kwa upande mwingine, Bw Sudi naye hataki siasa hizo ziingizwe ukabila ila mwaniaji maarufu ashinde kwa njia ya uwazi.

“Wapigakura wanafaa wawateme debeni viongozi wanaosisitizia ukabila na badala yake wawachague viongozi wenye kiu cha kuwapa maendeleo. Hakuna haja ya kuzingatia kuwa mmoja ni Mnandi, Mkeiyo au Mmarakwet,” akasema Bw Sudi.

You can share this post!

‘Sherehe’ kwa walevi baa 1,800 zikitakiwa kuuza...

Idara yajiandaa kushughulikia kesi tele za uchaguzi 2022