• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Idara yajiandaa kushughulikia kesi tele za uchaguzi 2022

Idara yajiandaa kushughulikia kesi tele za uchaguzi 2022

Na PHILIP MUYANGA

IDARA ya Mahakama inatarajia ongezeko la kesi za uchaguzi baada ya kura za mwaka ujao 2022 ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa Kamati Kuu Kuhusu Uchaguzi kwenye Idara ya Mahakama (JEC), yenye wajibu wa kushauri korti kuhusu njia ya kutatua kesi za uchaguzi upesi, kura ya mwaka 2022 itakuwa na ushindani mkubwa na wawaniaji wengi wanatarajiwa kufika mahakamani.

Suala hilo lilibainika katika warsha ambayo imekuwa ikiendelea katika hoteli ya Serena jijini Mombasa.

Kamati hiyo imekuwa ikiweka mikakati na kujadiliana kuhusu masuala kadhaa yanayogusia ufanisi wa uchaguzi mkuu ujao.

“Moja kati ya majukumu yetu ni kuwafundisha maafisa wetu wa mahakama, majaji, mahakimu, wafanyakazi wetu kuhusiana na masuala ya uchaguzi ili waendeshe kazi zao kwa kuzingatia sheria,” akasema Jaji Mohamed Ibrahim ambaye ni mwenyekiti wa JEC na pia Jaji wa Mahakama ya Juu.

JEC kwa ushirikiano na Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama itaandaa mafunzo kwa wahudumu wa mahakama kuhusu njia bora ya kusimamia uchaguzi pamoja na mbinu za kushughulikia kesi zitakazoibuka kuhusu uchaguzi huo.

Jaji Ibrahim pia alisema kuwa JEC itashirikisha wadau wengine kama Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT), Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) pamoja na maafisa wa polisi.

“Kazi yetu kubwa hasa huanza baada ya uchaguzi kufanyika ambapo huwa tunaanza kupokea malalamishi,” akasema Jaji Mohamed huku akisema JEC imekuwa ikiwajibika vyema katika chaguzi ambazo zimepita.

JEC pia inalenga kuorodhesha masuala yote yanayohitajika ili kila kesi ya uchaguzi isikizwe na kuamuliwa ipasavyo tena kwa uwazi.

JEC pia ina kamati ndogo ambayo inapiga msasa sheria husika kabla ya kutoa mapendekezo ambayo yatatumiwa kama msingi wa kusikiza kesi za uchaguzi baada ya 2022.

You can share this post!

Mvutano Bondeni wanasiasa wakiweka harakati za kugawana viti

PANDORA PAPERS: Marais wanavyokwepa ushuru na kuficha...