• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
NANI ATALIPA HAWA WAZITO?

NANI ATALIPA HAWA WAZITO?

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA huenda wakalazimika kulipa mamilioni ya pesa kugharamia kesi ya rufaa kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) baada ya mawakili 16 shupavu kuajiriwa kuwakilisha Rais Uhuru Kenyatta, Mwanasheria Mkuu na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Rufaa hiyo inalenga kubatilisha uamuzi wa majaji watano wa Mahakama Kuu uliositisha Mswada huo kwa misingi kuwa waasisi wake hawakuzingatia Katiba.

Majaji pia waliagiza IEBC kutoendesha kura ya maamuzi wakisema haina makamishna wa kutosha kufanikisha shughuli zake.

Ingawa gharama ya mawakili watakaowakilisha Rais Kenyatta IEBC na Mwanasheria Mkuu waliokuwa miongoni mwa washtakiwa katika kesi hiyo inatarajiwa kulipwa na mlipa ushuru, maswali yameibuka kuhusu atakayelipa mawakili watakaowakilisha ofisi ya kusimamia mchakato wa BBI ikizingatiwa kuwa mawakili nyota walioajiriwa hulipwa mamilioni ya pesa kwa huduma zao za kitaalamu, mbali na kuwakilisha wateja wao kortini.

Mawakili wote wa washtakiwa wanatarajiwa kuungana kushawishi Mahakama ya Rufaa kufuta uamuzi wa Mahakama Kuu hata ingawa wanawakilisha wateja tofauti.

Miongoni mwa mawakili ambao wanatarajiwa kumwakilisha Rais Kenyatta ni Gatonye Waweru, Mohammed Nyaoga na Desterio Oyatsi.

IEBC itawakilishwa na Profesa Githu Muigai na Eric Gumbo huku Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki akiwakilishwa na Wakili Mkuu George Oraro, Paul Nyamondi, Ken Nyaundi na Kamau Karori.

Bw Odinga ambaye pamoja na Rais Kenyatta walishtakiwa kwa kuasisi na kuendesha mchakato wa BBI atawakilishwa na saba shupavu akiwemo seneta wa Siaya James Orengo, mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, mshauri wake wa masuala ya sheria na katiba Paul Mwangi, Jackson Awele, Ben Shihanya na Arnold Oginga.

Bw Mwangi na Bw Shihanya ni miongoni mwa waandalizi wa Mswada wa BBI.

Ingawa kiasi cha pesa watakacholipwa ni siri kati ya kila mmoja na mteja wake, katika kesi za awali, mawakili wamekuwa wakilipwa mamilioni ya pesa kwa kuwakilisha wateja katika kesi muhimu kama za uchaguzi.

Kulingana na mawakili, mbali na kufika kortini kutetea wateja wao mbele ya majaji, huwa wanatoza ada za mamilioni kutoa huduma za kitaalamu.

“Baadhi yao hutoza mamilioni kadhaa kusoma stakabadhi za kesi na kutoa ushauri wa kitaalamu kabla ya kukubali kuwakilisha mteja na kisha hulipwa kwa muda wanaofika na kutumia kortini. Ikizingatiwa hadhi na tajiriba ya mawakili hao 16, ada zao zitakuwa mamilioni,” asema wakili mmoja aliyeomba tusitaje jina kwa sababu ya uhusiano wake wa kikazi na wenzake.

“Kesi hizi huchukua muda mwingu na nguvu nyingi wa mawakili kuziandaa na ndio sababu huwa wanatoza pesa nyingi kufidia muda ambao wangetumia kutoa huduma kwa wateja wengine,” asema.

Kwa kuwa IEBC na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni asasi za serikali, ni mlipa ushuru atakayelipa gharama ya rufaa ya BBI.

Katika kesi ambazo Rais Kenyatta hushtakiwa binafsi kama za uchaguzi, ni yeye huwa analipa mawakili kupitia ofisini ya kampeni zake.

Mawakili wanasema katika rufaa hii ya mswada wa BBI kila wakili atalipwa na mteja wake, lakini kuna uwezekano mlipa ushuru atabeba mzigo.

“Umekuwa mchakato wa serikali na zilikotoka pesa za kufadhili tangu 2018 ndiko zitatoka pesa za kulipa mawakili,” asema wakili mwingine.

Ripoti ya IEBC iliyowasilishwa bungeni 2018 ilionyesha kuwa tume ilitumia Sh202 milioni kulipa mawakili mwaka wa 2017 pekee.

Mnamo 2018, aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Ezra Chiloba aliambia wabunge kwamba walimlipa wakili Ahmednassir Abdullahi Sh40 milioni kwa huduma alizotoa kwa tume kwenye kesi ya kupinga matokeo ya urais 2013.

Katika kesi hiyo, wakili huyo aliwakilisha tume huku Aurelio Rebello aliyemwakilisha mwenyekiti wa IEBC akilipwa Sh30 milioni.

You can share this post!

Virusi vya corona vinavyohangaisha India vilizuka kitambo...

Fumbo kuhusu mauaji ya mfanyabiashara Bashir