• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Washirika wa Ruto wadai Uhuru na Raila wamemsaliti Kalonzo

Washirika wa Ruto wadai Uhuru na Raila wamemsaliti Kalonzo

NA PIUS MAUNDU

MWENYEKITI WA CHAMA cha United Democratic Alliance, Bw Johnson Muthama jana alisema kuwa umaarufu wa kiongozi wa Wiper eneo la Ukambani umeshuka kwa sababu alipuuza ushauri wake.

Akizungumza katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Iveti Kusini, Jonesmus Mwanza Kikuyu katika eneo la Kitulu, Machakos, Bw Muthama ambaye anagombea ugavana wa Kaunti ya Machakos, alisema alimweleza Bw Musyoka kuwa handisheki ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta ilinuiwa kumsaliti.

“Sasa wamemuacha. Nilimuonya kuwa muafaka kati ya Raila na Rais Kenyatta ulinuiwa kumfungia nje (ya urais),” alisema Bw Muthama.

Bw Musyoka alikubali kuunga Bw Odinga kugombea urais kwa mara ya tatu japo alikuwa amesisitiza ni waziri mkuu huyo wa zamani aliyefaa kumuunga mkono.

Katika hafla hiyo ya mazishi, wandani wa Dkt Ru – to kutoka Ukambani waliungana na washirika wa Bw Musyoka kumtaka Bw Odinga kumteua makamu huyo wa rais wa zamani kama mgombeaji mwenza.

Mbunge wa Machakos Mjini, Victor Munyaka jana alisema jamii ya Akamba ilimuunga mkono Bw Odinga mnamo 2013 na 2017 na mara hii anafaa tena kumtaja Bw Musyoka kama mgombeaji mwenza.

“Tulimpigia Raila kura 2013 na 2017. Ili kurudisha mkono na kwa kustahi jamii ya Akamba, anafaa kumteua Bw Musyoka kama mgombeaji mwenza ,” akasema Bw Munyaka.

Naye Seneta wa Kitui Enock Wambua na mwenzake wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr walisisitiza kuwa Bw Musyoka ndiye anayestahili kuwa mgombeaji mwenza wa Bw Odinga kutokana na makubaliano waliyokuwa nayo walipojiunga na Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

“Tulipotia saini mkataba na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, tulikuwa wazi kuwa Bw Musyoka atapokezwa wadhifa wa mgombeaji mwenza,” akasema Bw Kilonzo Jnr.

  • Tags

You can share this post!

Wafuasi watishia kuhama UDA baada ya uteuzi wa ukora

Nassir amshukuru Shahbal kwa kumwachia nafasi ya ugavana

T L