• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
NDC ya Jubilee kufanyika licha ya ‘vijimambo’

NDC ya Jubilee kufanyika licha ya ‘vijimambo’

NA BENSON MATHEKA

MKUTANO maalumu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) wa chama cha Jubilee utafanyika Jumatatu na Jumanne wiki ijayo ulivyopangwa licha ya chama hicho kukatazwa kutumia ukumbi wa Bomas, Nairobi, Naibu mwenyekiti wake David Murathe amesema.

Mnamo Jumatano, usimamizi wa Bomas uliarifu chama hicho kwamba ukumbi huo hautapatikana Jumatatu kwa mkutano ulioitishwa na kiongozi wake anayepigwa vita Uhuru Kenyatta, kwa kuwa umefungwa ili kufanyiwa ukarabati.

Barua ya Bomas kwa chama hicho ilizua wasiwasi wa kutofanyika kwa mkutano huo kwa kuwa maandalizi yalikuwa yamekamilika na ilani kutolewa kwa wajumbe wa matawi yote.

Hata hivyo, Bw Murathe aliondolea wajumbe wasiwasi akisema kwamba chama hicho kitatafuta ukumbi mwingine wa kufanyia mkutano kabla ya Jumatatu.

“Mkutano utafanyika ilivyotangazwa na kiongozi wa chama na kusisitizwa na katibu mkuu Jeremiah Kioni. Tutawaarifu wajumbe ukumbi mpya kabla ya Jumatatu kupitia tangazo,” Bw Murathe aliambia Taifa Leo.

Ili kuhakikisha wajumbe kutoka matawi yote hawakanganyikiwi, Bw Murathe alisema kila mmoja atatumiwa arafa ya kumwalika na kumfahamisha eneo mpya la mkutano.

Mkutano huo uliitishwa na Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta katika juhudi za kurejesha utulivu katika chama alichotumia kutawala mzozo wa uongozi ulipoibuka.

Makundi mawili moja linaloongozwa na Bw Kioni anayeungwa na Bw Kenyatta na linaloongozwa na mbunge maalumu Sabina Chege na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki yanazozania uongozi wa chama hicho.

Bi Chege ametwikwa wadhifa wa kaimu kiongozi wa chama na mrengo wake umejitenga na mkutano ulioitishwa na Uhuru jaribio ambalo mrengo wa Bw Kioni umepuuza.

Jana Alhamisi, tawi la Nakuru la chama hicho liliunga Uhuru na mrengo wake na kusisitiza kuwa litahudhuria mkutano maalumu wa kitaifa wa wajumbe Jumatatu ijayo.

Likiongozwa na mwenyekiti wake Joseph Gichuru na aliyekuwa mwenyekiti James Karimi na aliyekuwa spika wa Bunge la kaunti ya Nakuru Joel Kairu, wanasiasa hao waliunga NDC hiyo wakisema itarejesha utulivu katika chama hicho.

“Kongamano maalumu limeitishwa kwa sababu chama chetu kimevurugwa na Kenya Kwanza. Tunaunga kongamano hilo na tutahudhuria kupanga upya chama chetu. Kaunti ndogo zote za Nakuru zitawakilishwa katika mkutano huo,” alisema Bw Kairu.

“Chama cha Jubilee kingali imara, tunawaomba Wakenya wa nia njema kupuuza madai kwamba kimekufa,” aliongeza Bw Kairu.

  • Tags

You can share this post!

Mahasla kunywa chai bila sukari

Madoli ya ngono kuharibiwa na KRA

T L