• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Nderitu akatalia mbali ombi la PAA na MCCP la kutaka kujiondoa kutoka Azimio

Nderitu akatalia mbali ombi la PAA na MCCP la kutaka kujiondoa kutoka Azimio

NA CHARLES WASONGA

MSAJILI wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu amakataa maombi ya vyama vya Maendeleo Chap Chap (MCCP) na Pamoja African Alliance (PAA) kutaka kujiondoa kutoka muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Katika barua ya maafisa wa vyama hivyo viwili, Bi Nderitu alisema kuwa vyama hivyo vitaendelea kusalia kuwa wanachama wa Azimio kulingana na mkataba uliobuni muungano huo.

Alisema vyama hivyo havijafuata taratibu za kujiondoa zilizoko katika mkataba huo.

“Urejelee sehemu ya tatu ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa (PPA) na makubaliano ya muungano ya Azimio ili kuelewa taratibu zinazofaa kufuatwa na vyama kujiunga au kujiondoa kutoka muungano huo.

“Chini ya taratibu hizo, Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa haina mamlaka ya kuondoa PAA kutoka muungano wa Azimio kulingana na ombi lenu, bila kufuata kanuni zilizowekwa,” Bi Nderitu akasema kwenye barua kwa chama hicho kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi.

Msajili huyo alituma barua kama hiyo kwa maafisa wa chama cha MCCP kinachoongozwa na gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua.

Kulingana na mkataba wa kuundwa kwa Azimio uliotiwa saini na vyama 26 vilivyoko ndani ya muungano huo, hakuna chama kitaruhusiwa kujiondoa baada ya miezi tisa, tangu kusajiliwa kwake.

Mkataba huo unaeleza kuwa hakuna chama kinaweza kujiondoa miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Chama shirika ambacho kinataka kujiondoa kitaruhusiwa tu kufanya hivyo miezi mitatu baada ya uchaguzi huo mkuu.

Hata hivyo, chama cha kisiasa ambacho kinataka kujiondoa, kwanza kinahitajika kutoa notisi ya siku 90 kwa baraza kuu la Azimio, ambacho ni asasi ya pili yenye mamlaka katika muungano huo.

“Hakuna chama kinachoweza kujiondoa miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 au ndani ya miezi mitatu baada ya tarehe ya uchaguzi huo,” kipengele cha 22 cha mkataba huo kinasema, chini ya sehemu ‘Kujiondoa kwa Vyama’.

Mnamo Aprili 22, 2022 baadhi ya maafisa wa MCCP walimwandikia Msajili wa Vyama vya Kisiasa wakiomba kwamba chama hicho kiruhusiwe kujiondoa kutoka Azimio.

Maafisa hao walimsuta kiongozi wa chama hicho Dkt Mutua kwa kufeli kufuatia “utaratibu ufaao” kabla ya kuishirikisha chama hicho ndani ya Azimio.

“Kiongozi wa MCCP sio mmoja wa waliotia saini mkataba wa makubaliano,” wakasema katika barua kwa Bi Nderitu.

Maafisa hao walidai kuwa chama hicho hakikuitisha kongamano la wajumbe (NDC) kuidhinisha pendekezo la kujiunga na Azimio.

Lakini Bi Nderitu alisema kuwa MCCP ilitia saini mkataba wa kuundwa kwa Azimio na kwamba hana mamlaka ya kuidhini ombi la maafisa hao kwamba chama hicho kuruhusiwe kujiondoa kutoka muungano huo.

“Tayari Azimio ni chama cha muungano kilichosajiliwa kwa mujibu wa sehemu 7 (7) Sheria ya Vyama vya Kisiasa, 2022, na kanuni za 2019.

“Kwa hivyo, Msajili wa Vyama vya Kisiasa hana mamlaka ya kuidhinisha kujiondoa kulingana na ombi lenu, hadi pale taratibu zilizowekwa katika mkataba wa muungano huo zitafuatwa,” Bi Nderitu akasema.

Vile vile, Ijumaa iliyopita chama cha PAA kiliwasilisha ombi la kutaka kiruhusiwe kujiondoa Azimio

Chama hicho kilidai kuwa Kamati yake Kuu ya Kitaifa (NEC) haikuidhinisha mkataba wa kuundwa kwa Azimio.

Katika barua kilichoandikia Afisi ya Bi Nderitu mnamo Aprili 25, PAA kinasema kuwa kilipania kujiunga na muungano wala sio chama cha muungano.

Aidha, kinasema kuwa hakikupewa nakala za stakabadhi za mkataba wa kuundwa kwa Azimio.

Kwa hivyo, kulingana na chama hicho ambacho kina ufuasi mkubwa katika eneo la Pwani ya Kenya, kinahisi kutengwa na kutothaminiwa katika muungano huo ambao mgombeaji wake wa urais ni kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Kwa hivyo, mkutano wa baraza kuu la PAA uliofanyika Aprili 25, 2022 umeamua kufutilia mbali maktaba uliotiwa saini mnamo Aprili 5 ambao ulishirikisha PAA na Azimio,” PAA ikasema katika barua yake kwa Bi Nderitu.

Muungano wa Azimio, unaoshirikisha vyama 26 umekuwa ukikumbwa na misukosuko mbalimbali katika siku za hivi karibuni, ambayo imeathiri uthabiti wake.

Kando na juhudi za vyama vya PAA na MCCP za kutaka kujiondoa, Azimio inakabiliwa na kizungumkuti kuhusu uteuzi wa mgombea mwenza wa Bw Odinga na makubaliano kuhusu uteuzi wa wagombeaji maeneo mbalimbali nchini.

  • Tags

You can share this post!

Norwich City washushwa daraja katika EPL

Chelugui awarai wafanyakazi wadumishe amani msimu wa...

T L