• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 10:01 PM
Nilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha Lamu inakuwa na lami – Ruto

Nilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha Lamu inakuwa na lami – Ruto

NA KALUME KAZUNGU

NAIBU wa Rais, William Ruto aliendeleza majisifu yake kwa kutumia miradi ya serikali kuu ambayo utawala wake amekuwa akiusuta waziwazi.

Akihutubia umma kwenye uwanja wa Kamukunji ulioko mjini Witu wakati wa ziara yake Kaunti ya Lamu Ijumaa, Bw Ruto alishikilia kuwa ni kupitia uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na yeye kama Naibu wa Rais ambapo Lamu kwa mara ya kwanza tangu uhuru wa nchi hii kupatikana iliweza kujengwa barabara ya lami ya kilomita 135.

Ujenzi wa mradi huo uliogharimu serikali kuu kima cha Sh10.8 bilioni ulizinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi, 2017.

Ujenzi huo ulikamilika na kufunguliwa rasmi na kiongozi huyo wa taifa mnamo Mei 20, 2021, siku ambayo pia Rais Kenyatta alizindua rasmi shughuli kwenye bandari ya Lamu (Lapsset).

Kwenye mazungumzo yake, Bw Ruto alishikilia kuwa kupitia uongozi wa Rais Kenyatta na yeye, Lamu ilishuhudia kuimarika kwa miundomsingi ya afya, ikiwemo vifaa vya kisasa vya hospitali za King Fahd, Faza na Mpeketoni vilivyodhaminiwa na serikali kuu kupitia mradi wa MES.

Alisema ni kupitia uongozi wa Rais Kenyatta na yeye binafsi ambapo idadi ya watu waliounganishiwa nyumba zao na stima iliongezeka kutoka 3000 pekee hadi 27,000.

Naibu huyo wa Rais alimsuta mgombea urais kupitia mrengo wa Azimio One Kenya, Raila Odinga, akimtaja kuwa mtu wa vitendawili bila matendo na maendeleo yoyote.

“Nataka watu wa Witu leo mfahamu kuwa uchaguzi ujao si mashindano ya urembo bali ni kwa watu wachapa kazi. Mimi najivunia kuwa nilipoingia madarakani kama Naibu wa Rais tulihakikisha barabara ya Lamu inajengwa, hospitali zinaboreshewa miundomsingi na watu wengi zaidi hapa Lamu kuunganishwa kwa umeme,” akasema Bw Ruto.

“Sasa huyu mtu wa vitendawili ataka kushindana na mimi ilhali hana rekodi yoyote ya maendeleo hapa Witu na Lamu licha ya kuhudumia taifa hili kama Waziri Mkuu. Mnichague ili kuleta maendeleo zaidi Agosti 9, 2022,” akasema Bw Ruto.

Aliahidi kuboresha maisha ya wamama mboga, boda boda na watu wengine wa biashara ndogogo endapo atachaguliwa Rais wan chi hii.

Bw Ruto aliahidi kuwapunguzia wananchi gharama ya bima ya afya, ambapo badala ya kulipa Sh500 kwa mwezi ili kugharimikia NHIF, yeye atateremsha kiwango hicho hadi Sh300 pekee ilhali wale wasiojiweza kabisa wakibebewa gharama hizo na serikali.

Naye mgombea ugavana wa Lamu kupitia chama cha ANC na Kenya Kwanza, Issa Timamy aliwarai wananchi kumuunga mkono Bw Ruto na kuhakikisha ameshinda uchaguzi wa Agosti 9, 2022 ili kusaidia kutatua dhuluma za kihistoria ambazo eneo hilo imeshuhudia tangu uhuru wa Kenya kupatikana.

“Tukimchagua Bw Ruto atapigania kuhakikisha matatizo ya ardhi, ukosefu wa ajira na utelekezaji wa Lamu katika masuala yua kimsingi vinatatuliwa. Tushirikiane ili kuona kwamba ndoto hiyo inatimia,” akasema Bw Timamy.

Mgombea kiti cha useneta, kaunti ya Lamu kupitia UDA, Francis Mugo alieleza matumaini kuwa matatizo ya kimsingi ambayo vijana wa Lamu na Kenya wanakumbana nayo, ikiwemo ukosefu wa ajira na dawa za kulevya yatasuluhishwa endapo Bw Ruto atachaguliwa kuongoza taifa hili ifikapo Agosti 9.

Wengine walioandamana na Bw Ruto kwenye ziara ya Lamu ni Gavana wa Kwale, Salim Mvurya, Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale, miongoni mwa viongozi wengine wa mrengo wa Kenya Kwanza wa Ukanda wa Pwani.

  • Tags

You can share this post!

Equity kutoa huduma kupitia WhatsApp, Facebook, Telegram

VITUKO: Harusi tunayo! Staa Rashford avisha Lucia pete ya...

T L