• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Nitamshinda Raila 2027 – Ruto

Nitamshinda Raila 2027 – Ruto

NA WYCLIFFE NYABERI 

RAIS William Ruto amemtaka kinara wa ODM Raila Odinga asitishe maandamano na badala yake ampe nafasi awatimizie Wakenya ahadi alizotoa wakati wa kampeni.

Ruto akiwa kwenye ziara katika eneo la Gusii, amemsuta Bw Odinga kwa maandamano ya Jumatatu wiki jana hasa jijini Nairobi na Kisumu aliyosema yalisababisha uharibifu mkubwa wa mali, huku akisema mbinu hiyo ni chafu na si suluhisho katika kupunguza gharama ya maisha.

Rais amesema hata mrengo wa upinzani uandamane mara ngapi, serikali yake haitayumbishwa na maandamano yanayotishia utulivu nchini huku akidokeza asasi za polisi zitachukua kila hatua kuwalinda Wakenya dhidi ya uporaji unaofanyika wakati wa maandamano hayo.

“Hakuna jinsi tutakavyopunguza gharama ya maisha kwa kubeba sufuria na kuandamana. Tutapunguza gharama hiyo tu kwa kuwapa wakulima pembejeo za bei nafuu ili wazalishe mazao zaidi, na ikiwa tutapanga ajenda za vijana. Tayari tumeanza hayo,” Rais Ruto amesema.

Rais alitumia ziara hiyo pia kumweleza Bw Odinga kuwa yuko tayari kumenyana naye tena kwa kinyang’anyiro kingine mwaka 2027 ikiwa  atawania na akajipiga kifua kwamba atambwaga.

Amepuuzilia mbali madai ya Bw Odinga kwamba kuna mfichuzi (whistleblower) anayejua idadi kamili ya kura kila mwaniaji wa urais alizoa katika kinyang’anyiro cha mwaka 2022.

Amesema kauli hizo ni za uongo na hazina mashiko yoyote.

“Yule jamaa rafiki yangu anasema kuwa kuna whistleblower anayejua jinsi kura zilivyopigwa. Nataka kuwauliza hapa watu wa Kisii, ni nyinyi mlichagua viongozi au ni whistleblower? Si ni nyinyi mlichagua viongozi… basi hawa watu wanataka nini? Waniache niwafanyie kazi bwanaa,” akasema rais.

Dkt Ruto alitumia ziara hiyo kuwarai viongozi wa jamii ya Abagusii kuungana naye ili kuwafaidi raia kimaendeleo.

Mojawapo ya miradi aliyosema rais itawafaa wakazi wa eneo hilo ni kuanzishwa kwa ujenzi wa nyumba 10, 000 zenye bei nafuu alizosema zitatoa suluhisho kwa ugawanyaji wa vipande vya ardhi kutokana na idasi kubwa ya watu.

Katika ziara ya Alhamisi, Rais Ruto amezuru taasisi ya Kisii alikofungua maabara ya kidijitali.

Amezuru na kufungua mradi wa maji wa Kegati uliokamilishwa kwa kima cha Sh1.5 bilioni uliofadhiliwa kwa pamoja na benki ya Ujerumani na serikali kuu.

Kisha amefululiza na kufungua barabara ya Kemera-Magombo-Rigoma-Amabuko kabla ya kukagua mradi mwingine Sironga.

Alikuwa ameandamana na waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, magavana Simba Arati, Amos Nyaribo, wabunge pamoja na viongozi wengine.

Katika ziara yake ya siku ya pili, rais anatarajiwa kuhudhuria hafla ya kumkaribisha nyumbani Bw Machogu nyumbani kwake Gesusu tangu amteue waziri.

  • Tags

You can share this post!

Dereva ashtakiwa kumteka nyara polisi

Mwanahabari mkongwe apumzishwa

T L