• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 10:01 PM
‘Ochieng’ yuko hatarini kujizika kisiasa Nyanza’

‘Ochieng’ yuko hatarini kujizika kisiasa Nyanza’

NA KASSIM ADINASI

HATUA ya mbunge wa Ugenya David Ochieng’ na baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Luo Nyanza, kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza, inaonekana kama hatari kwa mustakabali wao kisiasa eneo hilo.

Hii ni kwa sababu kitendo hicho kimesawiriwa kama uasi dhidi ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye amekuwa na usemi mkubwa Luo Nyanza tangu kifo cha babake, Jaramogi Oginga Odinga mnamo 1994.

Mwanasiasa yeyote ambaye amewahi kumkaidi Raila hujipata pabaya kisiasa kwa kukataliwa na wapigakura.

Hii ndio hatari inayomkodolea macho Bw Ochieng’ na wanasiasa waliomtembelea Rais mteule William Ruto katika makazi yake rasmi mtaani, Karen, Nairobi juzi na kutangaza kujiunga na Kenya Kwanza.

Wanasiasa hao ni; aliyekuwa Gavana wa Kisumu Jack Ranguma, mbunge anayeondoka wa Kisumu Mjini Magharibi Olago Aluoch na seneta wa Kisumu anayeondoka Fred Outa.

Awali, aliyekuwa mbunge wa Rarieda Nicolas Gumbo alihama mrengo wa Azimio na kujiunga na kambi ya Kenya Kwanza, baada ya juhudi zake za kutwaa kiti cha ugavana wa Siaya kufeli aliposhindwa na mwanasiasa mkongwe James Orengo.

Aliwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha United Democratic Movement (UDM) kinachoongzwa na aliyekuwa Gavana wa Mandera Ali Roba.

Wanasiasa kutoka Nyanza wanaogura Azimio kujiunga na Kenya Kwanza wameelezea kukasirishwa na kile wanachotaja kama kudhulumiwa na chama cha ODM, kinachoongozwa na Bw Odinga.

Hata hivyo, Bw Ochieng’ ndiye mwanasiasa wa pekee ambaye alishinda kiti cha ubunge katika eneo la Luo Nyanza baada ya kuwania kwa tikiti ya chama chake cha Movement for Democratic and Growth (MDG).

Hii ni licha ya kwamba ODM ndicho chama maarufu zaidi katika eneo hilo.

Bw Ochieng’ alichaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2013 kwa tiketi ya ODM.

Lakini katika uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Ochieng’ alishindwa na Bw Christopher Karan wa ODM.

Hata hivyo, mahakama ilibatilisha ushindi wa Bw Karan kufuatia kesi iliyowasilishwa na Bw Ochieng’.

Mbunge huyo alimshinda Bw Karan katika uchaguzi mdogo uliofanyika mnamo Juni 29, 2019.

Chama cha MDG ni miongoni mwa vyama 26 vilivyotia saini mkataba wa kuunda muungano wa Azimio mapema mwaka huu 2022.

Katika uchaguzi wa Agosti 9 Bw Ochieng’ alitetea kiti chake cha ubunge kwa tiketi ya MDG.

Hata hivyo, Bw Ranguma ambaye aliwania ugavana wa Kisumu kwa tiketi ya chama hicho aliangushwa na gavana wa sasa Profesa Anyang Nyong’o.

Naye Bw Aluoch alibwagwa na Bi Rosa Buyu (ODM) katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha eneobunge la Kisumu Mjini Magharibi.

Wanasiasa wengine ambao walijaribu kumkaidi Bw Odinga na wakatemwa na wapigakura ni aliyekuwa mbunge wa Karachuonyo James Rege na wabunge wa zamani wa Rangwe Dkt Shem Ochuodho na Bw Martin Otieno Ogindo.

  • Tags

You can share this post!

Msichana, 15, akiri kuua ndugu zake 2 pamoja na binamuye

West Ham United wapepeta Aston Villa katika gozi la EPL

T L