• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
ODM: Raila si ‘kifaranga’ wa serikali

ODM: Raila si ‘kifaranga’ wa serikali

Na GEORGE ODIWUOR

VIONGOZI wa ODM wamemtaka Naibu Rais Dkt William Ruto akome kumrejelea Kinara wao Raila Odinga kama mradi wa serikali.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema ni vibaya kwa Dkt Ruto na wandani wake kudai Bw Odinga ni mradi ilhali waziri huyo mkuu wa zamani ameonyesha juhudi kwa kujisakia uungwaji mkono kutoka kwa raia kote nchini.

Dkt Ruto amekuwa akidai Bw Odinga anapigiwa upatu na serikali kutokana na ushirikiano wake wa karibu na Rais Uhuru Kenyatta baada ya wawili hao kuridhiana mnamo 2018.

Aidha, Dkt Ruto amenukuliwa mara kadhaa akimshambulia Bw Odinga kama aliyevuruga mpango wa utawala wa jubilee wa kuwahudumia Wakenya kupitia ‘handisheki’. Pia amedai kuwa Bw Odinga amekuwa akisaidiwa kufanya kampeni kwa kutumia rasilimali za serikali.

Hata hivyo, Bw Mbadi ambaye alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Homa Bay alisema kuwa Bw Odinga amepigania marekebisho mengi ya kiutawala nchini na mara hii ana nafasi nzuri ya kuingia ikulu 2022.

Kiongozi huyo wa wachache bungeni alidai kuwa kumrejelea Bw Odinga kama mradi wa serikali kunalenga kumsawiri kama kiongozi ambaye hawezi kusaka uungwaji mkono kivyake.

“Naibu Rais anafaa afahamu kuwa Bw Odinga ni mwanamageuzi ambaye amepigania nchi hii na kupitia mateso mengi licha ya kuwa ni mwanawe Makamu wa Rais wa kwanza wa Kenya,” akasema mbunge huyo wa Suba Kusini.

Mwenyekiti huyo wa ODM alimtaka Dkt Ruto ataje marekebisho aliyoyapigania huku akisema machungu ya kinara huyo wa UDA yanatokana na kugundua kuwa vuguvugu lake la Hasla haichangamkiwi tena na Wakenya.

“Msiwapigie kura wanasiasa ambao wanawagawanya. Naibu Rais na wandani wake wanaeneza siasa za ukabila na kumpaka tope Raila lakini hatafaulu kwa sababu Wakenya ni werevu na wanafahamu falsafa ya kiongozi wanayemtaka,” akasema.

Huku Dkt Ruto akivumisha vuguvugu lake la hasla, Bw Odinga naye amekuwa akiongoza mikutano ya Azimio la Umoja analosema linalenga kuwaunganisha Wakenya wote na kuwawezesha kuwachagua viongozi watakaowawajibikia vyema baada ya 2022.

Hata hivyo, maswali yameibuka kuhusu nani kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga ni mradi wa serikali, wanasiasa wa ODM wakisema kuwa kwa kuwa Dkt Ruto ni msaidizi wa Rais yupo pazuri kutumia rasilimali za serikali.

Kwa upande mwengine, Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale anasema kuwa ni dhahiri Rais Kenyatta na Dkt Ruto hawashirikiani kisiasa na sasa serikali inampendelea Bw Odinga.

Hata hivyo, wadadisi wanasema itakuwa hasara kubwa kwa Bw Odinga iwapo itabainika kuwa yeye ni mradi wa serikali na huenda hiyo ikayeyusha sifa zote ambazo amekuwa akijizolea kama mwanademokrasia na mpiganiaji wa haki za raia.

Ingawa viongozi wa OKA Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Gideon Moi pia wanatazamiwa kama wale ambao wataweza kutamba tu kama mradi wa serikali, mrengo wa Dkt Ruto unamwona Bw Odinga kuwa mpinzani mkuu na unaweka mikakati ya kumsawiri kama kiongozi anayeshabikiwa na utawala wa sasa ili kumpunguzia umaarufu.

You can share this post!

PSG na Marseille waumiza nyasi bure katika Ligi Kuu ya...

Seneta taabani tena kwa dai la kujeruhi mwanamke

T L