• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
ODM yashuku hila ugavana ukiahirishwa

ODM yashuku hila ugavana ukiahirishwa

NA VALENTINE OBARA

MGOMBEAJI ugavana Mombasa kupitia Chama cha ODM, Bw Abdulswamad Nassir, anataka uchunguzi ufanywe kuhusu hali iliyosababisha uchaguzi wa ugavana kuahirishwa kaunti hiyo.

Mbali na Mombasa, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliahirisha pia uchaguzi wa ugavana Kaunti ya Kakamega, maeneobunge ya Kacheliba, Pokot Kusini, Kitui Rural na Rongai (Nakuru).

Karatasi za kura ya ugavana Mombasa zilipatikana zimechapishiwa picha za wagombeaji wa Kilifi, huku zile za Kakamega zikipatikana na picha za wagombeaji wa Kirinyaga mnamo Jumatatu.

“Naambia IEBC kura zitamalizika na zikimalizika, uchunguzi utafanywa na ukweli utadhihirika wazi,” akasema mbunge huyo wa Mvita anayeondoka.

Bw Nassir aliibua shaka kuhusu utendakazi wa tume hiyo hasa ikizingatiwa kuwa, makamishna wake walikuwa wametumwa Ugiriki awali kuthibitisha uchapishaji wa karatasi za kura.

Uchapishaji ulifanywa na kampuni ya Inform Lykos (Hellas) SA iliyopewa kandarasi na IEBC.Awali, Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed, aliye pia katibu wa muungano wa Azimio, alitaka Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ichunguze uchapishaji wa karatasi zote za kura.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, ambaye sasa atalazimika kuendelea kuwa mamlakani hadi gavana mwingine achaguliwe, alisema matukio hayo yalishangaza.

Bw Joho na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, ni manaibu wa Bw Odinga katika ODM.

“Sijui ni sadfa aina gani inaweza kufika hivyo lakini la muhimu ni kwamba Mungu hakutaka leo tupige kura ya ugavana leo. Mimi naomba tuwe watulivu. Kwa mapenzi ya Mungu tutarudi tumchague gavana wetu,” akasema Jumanne.

Kwa upande wao, viongozi wa Kenya Kwanza katika Kaunti ya Mombasa wakiongozwa na aliyekuwa seneta, Bw Hassan Omar, anayewania ugavana kupitia kwa UDA, walisema IEBC iliwaarifu uchaguzi upya utafanywa baada ya wiki mbili zijazo.

Bw Omar alieleza masikitiko kuwa, wagombeaji kiti hicho wamepata hasara kubwa ya rasilimali nyingi walizokuwa wametumia kwa kampeni huku baadhi ya wapigakura wakisafiri kutoka mbali kuja kuchagua viongozi wao.

“Natumai siku hiyo wakiandaa uchaguzi Mombasa na Kakamega wananchi watapewa likizo ili wajitokeze kwa wingi,” akasema.

Pande zote zilieleza wasiwasi kwamba idadi ya wale watakaopiga kura ya ugavana itakuwa ndogo.Wiki mbili zilizopita, IEBC ilieleza kuwa wajumbe wake pamoja na wawakilishi wa vyama na mashirika mengine waliosafiri hadi Ugiriki waliridhishwa na uchapishaji kura.

Taarifa hiyo iliyotiwa sahihi na Naibu Mwenyekiti wa IEBC, Bi Juliana Cherera, na wawakilishi wa chama cha muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Kenya Kwanza na Baraza la Ushirikiano wa Kidini nchini (IRCK) ilitoa maelezo kuonyesha wadau waliridhishwa na uwezo wa kampuni ya Inform Lykos (Hellas) SA.

Jumanne, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli, aliibua upya mjadala kwamba karatasi za kura zinafaa ziwe zikichapishwa humu nchini.

Bw Atwoli alisema changamoto zilizotokea ni za kiufundi na IEBC huenda haikufahamu, lakini akasisitiza kuna mashirika mengi humu nchini ikiwemo kituo cha uchapishaji wa hati za serikali ambayo yanaweza kufanya kazi hiyo.

Kulingana naye, dosari hizo zingekuwa zimerekebishwa haraka kama karatasi zingechapishwa ndani ya nchi.

  • Tags

You can share this post!

Mshangao jina la Ngilu kuwa debeni

Wazee watatizika mitambo ikishindwa kunasa alama za vidole

T L