• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:21 PM
Pigo kwa ODM wabunge wawili wakipoteza viti vyao

Pigo kwa ODM wabunge wawili wakipoteza viti vyao

ALEX KALAMA Na JURGEN NAMBEKA

CHAMA cha ODM kimepata pigo baada ya mahakama kubatilisha uchaguzi wa wabunge wake wawili.

Mahakama Kuu ya mjini Malindi ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa mbunge wa Magarini, Bw Harrison Gharama Kombe.

Hayo yakijiri mahakama Kuu pia ilitupilia mbali ushindi wa mbunge wa Lagdera Bw Abdikadir Hussein, aliyekuwa ametajwa mshindi katika uchaguzi wa 2022 kupitia chama cha ODM.

Akitoa uamuzi wa kufutilia mbali ushindi wa Bw Kombe, jaji wa mahakama hiyo, Bw Alfred Mabeya, alieleza kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na hitilafu za kiuchaguzi.

Kulingana naye, shughuli ya kuhesabu kura ilikumbwa na utata hata kabla ya afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kumtangaza Bw Kombe mshindi.

Mahakama ilieleza kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu kwa njia kadhaa. Kati ya njia zilizotumika ni ile ya kuongeza karatasi za kupiga kura kwenye masanduku ya kupigia kura, kupunguza kura za washindani, pamoja na kubadilisha matokeo ili kumpendelea Bw Kombe.

Mahakama hiyo iliagiza IEBC eneo hilo kuandaa upya uchaguzi wa eneobunge hilo, kama inavyotakikana kulingana na sheria ya humu nchini.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na aliyekuwa mgombeaji wa kiti hicho kupitia kwa tiketi ya chama cha UDA, Bw Stanley Kenga pamoja na Michael Kingi wa PAA.

Katika uchaguzi huo, Bw Kombe alitangazwa kupata kura 11,946 huku Bw Kenga akimfuata na kura 11,925. Kulingana na matokeo hayo ya uchaguzi, Bw Kombe alikuwa ameshinda kwa kura 21 pekee.

Wawili hao walifuatiwa kwa karibu na Bw Michael Kingi wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) aliyekuwa na kura 7,921.

Bw Kombe alikuwa amejifufua kisiasa kwa kuingia katika bunge la 13, baada ya kupigwa na kibaridi nje ya uongozi kwa miaka mitano.

Katika kesi ya Bw Hussein iliyowasilishwa mahakamani na mshindani wake Bw Abdiqani Zeitun, aliyewania kiti cha eneobunge hilo kupitia kwa chama cha UDA, mahakama ilikuwa imeamuru IEBC kuhesabu upya kura za eneobunge hilo, mnamo Februari.

Katika uchaguzi huo, Bw Hussein alitangazwa mshindi kwa kura 5,939, dhidi ya Zeitun aliyepata kura 4,863.

Baada ya kutangazwa mshindi, Bw Hussein alieleza kuwa alikuwa ameuona mkono wa Mungu katika uchaguzi huo.

“Koo zina nafasi muhimu katika siasa za eneo letu. Nilichaguliwa licha ya kutoka kwenye ukoo mdogo. Sina maneno ya kutosha ya kuwapa shukrani,” alisema Bw Hussein.

Kwa sasa wakazi wa eneobunge la Lagdera watalazimika kurudi debeni kama tu wale wa eneobunge la Magarini, ili kuchagua mbunge wao.

Wakati uo huo, mahakama kuu imedumisha ushindi wa gavana wa Wajir, Bw Ahmed Abdullahi baada ya kutupa kesi ya kupinga ushindi wake.
Kulingana na Jaji George Dulu, upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kuwa gavana Abdullahi aliyechaguliwa kupitia ODM, hakuchaguliwa kwa njia halali.
  • Tags

You can share this post!

Form ni kuoga na kurudi soko, Edday mke wa Samidoh ashauriwa

Kaunti yafadhili 300 kuhudhuria mazishi ya mzee wa jamii ya...

T L