• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
Raila afafanua jinsi atakavyobadilisha uchumi wa Pwani

Raila afafanua jinsi atakavyobadilisha uchumi wa Pwani

NA VALENTINE OBARA

CHAMA cha kisiasa cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, kimelenga kuleta mabadiliko katika sekta kadha zinazogusia uchumi wa Pwani moja kwa moja.

Manifesto iliyozinduliwa rasmi na mwaniaji urais wa muungano huo, Bw Raila Odinga, inaonyesha mipango ya kurekebisha sekta kama vile za utalii, uchumi wa baharini unaojumuisha biashara za uvuvi na bandari, na utatuzi wa changamoto za ardhi ni miongoni mwa zile ambazo zitanufaisha eneo la Pwani kwa kiwango kikubwa endapo mipango hiyo itatekelezwa.

Ijapokuwa manifeso ni mwongozo wa mipango ya kitaifa inayokusudiwa kutekelezwa endapo Bw Odinga atashinda urais, sekta hizo zimekuwa na changamoto tele kwa uchumi wa Pwani ikilinganishwa na maeneo mengine nchini.

Katika suala la ardhi ambalo limekuwa donda sugu kwa miaka mingi, manifesto hiyo imerejelea hitaji la kurekebisha historia ya ukiukaji wa haki za umiliki wa ardhi kwa wenyeji wa Pwani na maeneo mengine nchini.

Ili kutatua tatizo hili, manifesto hiyo inapendekeza mtindo ambapo serikali itakuwa ikinunua ardhi ambapo maskwota wanaishi ili kuwagawia.

“(Tunajitolea) kuzipatia ardhi familia zisizomiliki ardhi na maskwota eneo la Pwani na maeneo mengine ya nchi kupitia kwa ununuzi wa sehemu kubwa za ardhi na kutoa makao kwa familia zilizoathirika na maskwota,” sehemu ya manifesto hiyo iliyotolewa rasmi Jumatatu usiku inasema.

Mpango sawa na huu umekuwa ukipigiwa debe na Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais, Dkt William Ruto, kila anapofanya kampeni zake ukanda huo.

Kuhusu uchumi wa baharini, Azimio inalenga kurekebisha sera zinazosimamia sekta za uvuvi, utalii wa baharini, uchukuzi wa bandarini na usafiri wa vyombo vya baharini.

Mbali na kufanyia marekebisho sera, ahadi imetolewa pia kuongeza fedha za utafiti kuhusu uchumi wa bahari, na kuwaongeza uwezo jamii zinazotegemea uvuvi kiriziki.

Manifesto hiyo inasema wavuvi watafadhiliwa kuwa na boti za kisasa, vyombo vya kisasa vya uvuvi na kila eneobunge linalotegemea uvuvi litajengewa sehemu ya kuhifadhi samaki.

Utekelezaji wa mipango iliyoanzishwa kupanua Bandari za Mombasa na Lamu umepangiwa kukamilishwa kwa haraka, sawa na ujenzi wa maeneo maalumu ya kiviwanda ya Dongo Kundu na Bandari ya Lamu.

Mbali na hayo, Bw Odinga ameahidi kwenye manifesto yake kuwa endapo atafanikiwa kurithi kiti cha Rais Uhuru Kenyatta, utawala wake utawekeza katika upanuzi wa taasisi zinazotoa mafunzo kuhusu masuala ya baharini na uhasibu wa vyombo vya baharini.

“Hii itawezesha Kenya kuwa na rasilimali za kimataifa za masuala ya baharini,” ikaeleza manifesto hiyo.

Kuhusu utalii uliofifia katika miaka iliyopita hadi sasa, Azimio inalenga kuhimiza wadau kuongeza vivutio ili kujumuisha utalii wa kisanaa, michezo, mikutano, matibabu, kibiashara, tamaduni miongoni mwa mengine ambayo huwa hayapewi uzito kwa kiasi kinachostahili.

Muungano huo pia umelenga kuhimiza mataifa ya kigeni kubadili ilani zinazotolewa mara kwa mara za kuonya raia wao kuhusu usalama Kenya, mbali na kuwawezesha raia wa Kenya kutalii maeneo nchini. ili kukuza utalii wa ndani kwa ndani.

Akihutubu wakati wa uzinduzi wa manifesto hiyo, Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed, alisema yaliyomo kwenye mwongozo huo yalikusanywa kutoka kwa maoni ya wananchi katika maeneo tofauti ya nchi.

  • Tags

You can share this post!

TZ yatia mkataba kufunza Kiswahili katika nchi tatu

Kithi apuuza madai ya kujiondoa na kumuunga Jumwa ugavana

T L